Waziri Mchengerwa atoa miaka mitatu kwa Ocean Road,wagonjwa wa saratani kutibiwa nchini

DAR-Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameipa Bodi ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) muda wa miaka mitatu kuhakikisha hakuna Mtanzania anayekwenda nje ya nchi kutibiwa saratani.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo Januari 5, 2026 wakati wa uzinduzi wa Bodi ya ORCI, uzimduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam.

"Tanzania chini ya Serikali ya awamu ya Sita ya Mhe. Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa na sasa ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye huduma za kisasa za matibabu ya saratani, hivyo lazima tuende na kasi ya Mhe. Rais," amesema Mhe. Mchengerwa.
Kabla ya uzinduzi huo Waziri Mchengerwa, alikagua miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na taasisi hiyo ikiwemo ufungaji wa mashine tatu mpya za matibabu ya saratani aina ya LINAC na Cobalt, upatikanaji wa mashine za kisasa za uchunguzi na matibabu ikiwemo PET CT, pamoja na uanzishaji wa kinu cha kuzalisha dawa za nyuklia (Cyclotron) kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

Aidha, Waziri amekagua ujenzi wa jengo jipya la huduma za kimataifa linalolenga kuboresha huduma kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi huku akipongeza Menejimenti ya ORCI kwa utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Desemba, 2025 ya kuhakikisha mashine tatu za uchunguzi wa PET zinafungwa na kuanza kutoa huduma.
Katika ziara hiyo, Waziri Mchengerwa amezungumza na wagonjwa waliokuwa wakipatiwa huduma, ambapo kwa niaba yao Bi. Justina Allen amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za tiba ya mionzi na kusema kwa sasa wagonjwa wasio na uwezo wanapata matibabu bure baada ya kufuata taratibu zilizowekwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo, amesema kukamilika kwa ufungaji wa mashine mpya kutapunguza muda wa kusubiri huduma kutoka wiki 20 hadi takriban ni wiki mbili na kuongeza kuwa idadi ya wagonjwa wanaopata huduma kwa siku itaongezeka kutoka 200 na kufikia hadi zaidi ya 400.
Hata hivyo, Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa mageuzi ya huduma za saratani hayaishii kwenye majengo au mashine pekee, bali yaanze kwenye usanifu bora wa utoaji huduma kwa mgonjwa na kuboresha uzoefu wake wote wa matibabu na kuitaka ORCI kuwa wabunifu, jasiri na kuvunja mazoea ya zamani ili kuwa kituo cha ubora barani Afrika.

Sambamba na hayo Mhe. Mchengerwa amesisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa, mifumo ya kielektroniki ya taarifa za wagonjwa na usimamizi thabiti wa Bodi, sambamba na kuimarisha utafiti na ushirikiano wa kitaifa na kimataifa, ili kuifanya ORCI kuwa taasisi inayoongoza katika matibabu na utafiti wa saratani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here