DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila amesema kuwa, mifumo ya malipo ya Taifa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi jumuishi na kuimarisha ujumuishwaji wa kifedha nchini.
Akitoa hotuba ya ukaribisho kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Biashara (MBA) kutoka Chuo Kikuu cha Stanford, Marekani waliotembelea BoT jijini Dar es Salaam, Dkt. Kayandabila ameeleza kuwa,mifumo ya malipo inachangia ukuaji wa uchumi shirikishi kwa kuwezesha malipo ambayo yanachochea ugavi katika uchumi na kuwa uti wa mgongo wa Uthabiti wa Sekta ya Fedha.
Amebainisha kuwa, mifumo ya malipo yenye ufanisi, iliyo salama na shirikishi huchochea ufanisi wa sera ya fedha kwa kuwezesha uenezaji mzuri wa mabadiliko ya viwango vya riba vya Benki Kuu na kuimarisha udhibiti wa ukwasi ndani ya uchumi.
Dkt.Kayandabila amesema Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kuwekeza katika miundombinu ili kuimarisha na kuboresha mifumo ya malipo, sambamba na kuchochea ubunifu hususan katika huduma za kifedha za kidijitali na ujumuishwaji wa kifedha.
Akifafanua kuhusu historia ya maboresho hayo, alisema kuwa mchakato wa kisasa wa mifumo ya malipo ulianza katikati ya miaka ya 1990 kama sehemu ya mageuzi mapana ya sekta ya fedha yaliyolenga kuongeza ufanisi, usalama na uthabiti wa mfumo wa fedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Bi. Lucy Shaidi, akielezea hatua muhimu zilizofikiwa katika safari ya kuendeleza mifumo ya malipo hadi kufikia mwaka 2025 amesema kuwa, kumekuwapo na ukuaji wa kasi wa malipo ya papo kwa papo, huduma za fedha kupitia simu za mkononi, pamoja na mifumo ya malipo inayoweza kuunganishwa.
Alibainisha kuwa,maendeleo hayo yanaendelea kuichochea Tanzania kuelekea katika mfumo wa fedha uliojumuishi zaidi, wenye ufanisi, na unaotegemea kwa kiasi kikubwa teknolojia za kidijitali.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya Benki Kuu katika mifumo ya malipo ni kuanzishwa kwa Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Hapo (Tanzania Instant Payment System-TIPS) unaoruhusu watumiaji wa huduma za fedha kutuma na kupokea fedha papo hapo, bila kujali taasisi ya kifedha wanayotumia.










