MOROGORO-Mahakama ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro imemhukumu Hamadi Mohamed Mangomba (35), mkazi wa Melela–Mlandizi wilayani Mvomero, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilogramu 38.22.
Hukumu hiyo ilitolewa Machi 18, 2026 na Hakimu Mkazi T. J. Yamungu katika kesi ya jinai Na. 29850/2025, chini ya kifungu cha 16(1) na (2)(c) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 (Marejeo ya 2023), baada ya mahakama kuridhika kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashitaka ulithibitisha hatia ya mshtakiwa bila kuacha shaka.
Mshtakiwa alikamatwa Novemba 15, 2025 katika eneo la Melela–Mlandizi na maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kufuatia taarifa za kiintelijensia, akiwa akisafirisha bangi hiyo kwa kutumia pikipiki yenye namba MC 170 FAX, ikiwa imehifadhiwa ndani ya mifuko miwili. Uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali ulithibitisha kuwa dawa hizo ni bangi.
Mahakama iliamuru dawa hizo kuteketezwa kwa mujibu wa sheria, huku mshtakiwa akiwa na haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30. Hukumu hii inaendeleza msimamo wa Serikali kupitia DCEA katika kudhibiti na kupambana na biashara ya dawa za kulevya nchini.
Tags
Bangi
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
