NA DIRAMAKINI
MTUMISHI wa Mungu wa huduma ya Embassy of God for All Nations, Prophet IPM amesema, mwaka 2026 unapaswa kuwa mwaka wa wanaume kujitathmini kwa kina na kuchukua hatua madhubuti za kujikwamua kiuchumi, licha ya changamoto mbalimbali za maisha wanazokabiliana nazo katika jamii ya sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Machi 3, 2026, Prophet IPM alisema, wanaume wengi wamekuwa wakibeba majukumu makubwa katika familia na jamii, huku wakikosa majukwaa au fursa za kueleza changamoto wanazopitia.
Alieleza kuwa, hali hiyo imechangia baadhi yao kufanya maamuzi magumu ambayo wakati mwingine huathiri ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kidini, ni muhimu kwa wanaume kupewa nafasi ya kujadiliana, kushirikishana uzoefu na kupata hamasa itakayowasaidia kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii.
“Ni wakati wa mwanaume kusimama na kujiuliza anachopaswa kufanya ili kuboresha maisha yake na ya familia yake. Ndiyo maana mwaka huu tumepanga kukutana kwa pamoja ili kujadili masuala muhimu yanayowahusu wanaume,” alisema Prophet IPM.
Alifafanua kuwa, katika kutekeleza lengo hilo, wameandaa kikao kikubwa kitakachowakutanisha wanaume kutoka maeneo mbalimbali kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea. Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika Aprili 2, 2026 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Prophet IPM alieleza kuwa, kongamano hilo litatoa fursa kwa wanaume kujifunza, kubadilishana mawazo na kupata motisha kutoka kwa watu wenye uzoefu katika sekta mbalimbali za maisha, hususan katika masuala ya ujasiriamali, uongozi na maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, alisema kiingilio cha kushiriki kongamano hilo kitakuwa shilingi 50,000 kwa kila mshiriki, ambapo pia waandaaji wamepanga kuwapatia washiriki chakula cha mchana wakati wa tukio hilo.
Katika hatua nyingine, Prophet IPM alibainisha kuwa licha ya taasisi yake kuwa na ibada maalum ya kukutanisha wanaume, mwaka huu wameamua kupanua wigo kwa kuwakaribisha wanaume wa dini zote ili kujenga mshikamano na kutoa jukwaa pana la kujadili changamoto zinazowakabili wanaume katika jamii.
“Tumelenga kuwaleta pamoja wanaume bila kujali tofauti zao za kidini au kijamii, ili kwa pamoja tujadili namna bora ya kukabiliana na changamoto za maisha na kuimarisha ustawi wa familia na taifa,” aliongeza.
Miongoni mwa wageni waalikwa katika kongamano hilo ni mfanyabiashara na bilionea Said Lugumi, pamoja na mashekhe na wafanyabiashara wengine wakubwa nchini.
Akizungumza kwa njia ya simu, Lugumi alithibitisha kushiriki kwake katika mkutano huo na kueleza kuwa atakuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu.
Alisema atatumia nafasi hiyo kuwatia hamasa vijana kutumia muda wao kwa tija na kuwekeza katika shughuli za maendeleo ili kujikwamua kiuchumi.
Alisisitiza kuwa, vijana wanapaswa kuwa na nidhamu ya kazi, ubunifu na uthubutu katika kutafuta fursa mbalimbali za kiuchumi ili kukabiliana na changamoto za maisha.
Kwa mujibu wa waandaaji wa tukio hilo, washiriki wote wanatakiwa kuzingatia mavazi rasmi yatakayovaliwa siku hiyo ambayo ni suti nyeusi, shati jeupe, tai nyekundu, soksi nyeusi pamoja na viatu vyeusi.
Aidha,kongamano hilo linatarajiwa kuvutia idadi kubwa ya wanaume kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, huku likilenga kutoa jukwaa la majadiliano na hamasa kwa wanaume ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa familia zao na taifa kwa ujumla.
.jpeg)