NA LWAGA MWAMBANDE
LUGHA za asili ni sehemu muhimu ya utambulisho na utamaduni wa jamii. Kupitia lugha hizi, historia, mila, desturi na maarifa ya jadi hupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Hivyo, lugha za asili si chombo cha mawasiliano tu, bali pia ni hazina ya urithi wa kitamaduni.
Aidha, lugha za asili huimarisha mshikamano wa jamii na kuwafanya watu wajivunie asili na utambulisho wao. Kupotea kwa lugha kunaweza kusababisha kupotea kwa baadhi ya maarifa na maadili ya jamii husika.
Mshairi wa Kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kutokana na changamoto za utandawazi na kuongezeka kwa matumizi ya lugha za kigeni, kuna umuhimu mkubwa wa kuchukua hatua za kulinda na kuendeleza lugha za asili.
Jamii, serikali na taasisi za elimu zinapaswa kushirikiana kuhimiza matumizi na ufundishaji wa lugha hizi ili kuhakikisha urithi wa kitamaduni unaendelea kudumu kwa vizazi vijavyo.Endelea;
1. Nafasi ya lugha mama, hivi ndiyo inakufa?
Kizaramo wanasema, kinakaribia kufa?
Hii si habari njema, twapoteza maarifa,
Lugha asili ni mali, ni utamaduni wetu.
2. Kujua lugha ya mama, ni kukuza maarifa,
Mbele unaposimama, na wa kwenu wewe refa,
Lakini sasa ni noma, lugha zetu zinakufa,
Lugha asili ni mali, ni utamaduni wetu.
3. Kiswahili twakisema, lugha yetu ya taifa,
Shuleni tunakisoma, twaongeza maarifa,
Ila kile chaniuma, lugha za jadi zakufa,
Lugha asili ni mali, ni utamaduni wetu.
4. Baba Nyerere lisema, manufaa yamekufa,
Kutambika kwenye boma, ndiyo imebaki sifa,
Ya kwake aliyasema, ninalia lugha kufa,
Lugha asili ni mali, ni utamaduni wetu.
5. Kiswahili chetu chema, duniani kina sifa,
Na lugha asili njema, kwa taifa na tarafa,
Zinatunza mengi mema, sio vizuri zikifa,
Lugha asili ni mali, ni utamaduni wetu.
6. Kuna mambo kuyasema, lugha ngeni huwa ufa,
Vile unavyoyasema, ni anguko la kifafa,
Hata zetu nyingi ngoma, kwa kilugha huwa sifa,
Lugha asili ni mali, ni utamaduni wetu.
7. Kichaga na Kisukuma, hizo zinakwenda kufa,
Kama tusipochagama, kuzidi kuziba nyufa,
Vita siyo lelemama, wenyewe ndio marefa,
Lugha asili ni mali,ni utamaduni wetu.
8. Faragha kitaka sema, hakuna panda ghorofa,
Lugha yetu tunasema, tunazoza kitarafa,
Wageni hawatasoma, akiliyo ishakufa,
Lugha asili ni mali, ni utamaduni wetu.
9. Ukabila tushatema, twazidisha utaifa,
Huko nyuma tumegoma, lugha kuujenga ufa,
Tutazidi kusimama, Jeremia na Zulfa,
Lugha asili ni mali, ni utamaduni wetu.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
.jpeg)