TANESCO yazindua ndege nyuki (drones) kuboresha ukaguzi wa miundombinu ya umeme nchini

DAR-Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO, limezindua rasmi matumizi ya ndege nyuki (drones) kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa njia za kusafirisha na kusambaza umeme ikiwa ni hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kupunguza muda wa kutatua changamoto za kukatika kwa umeme.
Uzinduzi huo umefanyika tarehe 17 Machi 2026 katika Ofisi za TANESCO, Ubungo jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Bw. Lazaro Twange.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bw. Twange amesema TANESCO inasimamia mtandao mkubwa wa miundombinu ya umeme nchini unaohitaji ufuatiliaji wa karibu kwa kutumia teknolojia za kisasa.
"Tuna njia za kusafirisha umeme ambazo zimetembea urefu wa takribani kilomita 8,500, na tuna njia za kusambaza umeme ambazo zimetembea karibu kilomita 200,000. Njia hizi zimepita ardhini kwenye mapori, pembezoni mwa barabara na maeneo yetu,” amesema Bw. Twange.

Ameeleza kuwa, jukumu la msingi la Shirika hilo ni kuhakikisha wateja wanapunguziwa muda wa utatuzi wa pale changamoto za umeme zinapojitokeza na kuhakikisha huduma inarejea kwa wakati wote.

“Kazi yetu ya kuhudumia wateja, moja ya kitu tunachopambana nacho zaidi ni kuhakikisha wateja wanapata umeme. Leo tumeanza safari ya mapinduzi ya teknolojia ya kuturahisishia kufanya kazi zetu,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Bw. Twange, pamoja na uwepo wa mifumo ya kubaini hitilafu, bado kulikuwa na changamoto ya kutambua eneo halisi la tatizo kwa haraka.

Amebainisha kuwa ndege nyuki (drones) zitasaidia kufanya ukaguzi wa haraka na wa kina kabla ya hitilafu kutokea.

“Leo tunazindua utaratibu huu mpya wa kutumia vifaa hivi aina ya ndege nyuki (drones) ambazo zimewekwa mifumo maalum ya kufuatilia miundombinu yetu ya umeme ili kugundua hali ya njia zetu kabla madhara hayajatokea,” ameeleza Bw. Twange

Aliongeza kuwa hatua hiyo pia itapunguza gharama na muda uliokuwa ukitumika awali katika ukaguzi wa kawaida.
“Hiki kitu kilikuwa kinatumia muda mrefu sana na kinatumia gharama kubwa kiasi.Timu zetu zilikuwa zinazunguka na magari, lakini sasa tutatumia muda mfupi kufanya ukaguzi kabla tatizo halijatokea,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kibamba, Salma Yahaya alisema matumizi ya ndege nyuki (drones) yatakuwa suluhisho la changamoto za muda na ugumu wa kufikia baadhi ya maeneo wakati wa ukaguzi.

“Ni mfumo utakaoturahisishia kuwapa wateja huduma kwa haraka. Tulikuwa tunatumia muda mwingi kufanya ukaguzi. Tulikuwa tunaenda kwa miguu kila nguzo, lakini kwa mfumo huu tutaweza kuona matatizo kwa urahisi na kupanga mpango kazi wa kuyatatua ili wateja wetu wasikose umeme,” amesema.

Uzinduzi wa matumizi ya ndege nyuki (drones) unaashiria mwendelezo wa hatua muhimu za mageuzi ya Shirika kutumia njia za kidijitali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme iliyo bora ndani ya wakati na endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here