NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali pamoja na kumpangia kituo balozi mmoja, katika hatua inayolenga kuimarisha ufanisi wa taasisi za umma na uwakilishi wa nchi nje ya mipaka yake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, uteuzi huo unahusisha nafasi mbalimbali za uongozi katika taasisi za Serikali na bodi zake.
Katika uteuzi huo, Bw. Adam Joseph Mrisho ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), akitarajiwa kuongoza juhudi za kitaifa za kudhibiti na kupambana na maambukizi ya UKIMWI nchini.
Aidha, Balozi Profesa Elizabeth Kiago Kiondo ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania, akichukua nafasi ya Profesa Rwekaza Sympho Mukandala ambaye amemaliza muda wake wa uongozi.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amempangia kituo Balozi Noel Emmanuel Kaganda kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Korea, ambapo ataiwakilisha Tanzania katika masuala ya kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa.
