NA GODFREY NNKO
BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua kampeni maalum ya 'I had a Dream' (Nilikuwa na Ndoto) inayolenga kuwawezesha Watanzania kufikia ndoto zao kwa kuwapatia suluhisho sahihi la kifedha, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ustawi wa jamii.
Kampeni hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa makundi mbalimbali ya wananchi, hususani wajasiriamali, wakulima na biashara ndogo na za kati, kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kupanua fursa za ajira nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Machi 18,2026 jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TCB Bank, Kaimu Mkurugenzi, Bw.Jema Msuya amesema, benki hiyo imejipanga kuwa mshirika wa maendeleo kwa wateja wake kwa kuwapatia huduma zinazokidhi mahitaji yao na kusaidia kufanikisha malengo ya kifedha.
"Tunataka kuwa karibu na wateja wetu na kuhakikisha kila Mtanzania anapata msaada wa kifedha unaomwezesha kufikia ndoto zake,” amesema.
Msuya amesema kuwa, lengo kuu la taasisi hiyo ni kujijengea nafasi si tu kama mtoa huduma za kifedha, bali pia kama mshirika wa maendeleo kwa wateja wake.
Ameeleza kuwa,kila Mtanzania mwenye ndoto au malengo anastahili kupata msaada stahiki wa kifedha ili kufanikisha malengo yake, akisisitiza kuwa changamoto kubwa kwa wengi si ukosefu wa mawazo au mipango, bali ni upungufu wa huduma sahihi za kifedha.
Aidha, Msuya amebainisha kuwa, kuwawezesha wajasiriamali mmoja mmoja kuna mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya jamii kwa ujumla, hususani kupitia ukuaji wa biashara ndogo na za kati pamoja na kuboresha ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa TCB Bank, Alex Dwashi amesema, kampeni hiyo inalenga kujenga uhusiano wa karibu na wateja kwa kuelewa changamoto zao na kutoa suluhisho mahsusi yatakayosaidia kukuza shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali.
“Kampeni hii inalenga kugusa maisha ya Watanzania moja kwa moja kwa kuwaunga mkono katika safari ya kukuza shughuli zao za kiuchumi,” amesema na kuongeza kuwa,
"Kampeni hii inahakisi kile ambacho sisi kama taasisi na nafasi tunayoithamini kuwa nayo katika maisha ya watu na jamii nzima ya Watanzania."
Ameeleza kuwa, Tanzania ni kitovu cha ndoto nyingi zinazosubiriwa kugeuzwa kuwa kweli, hivyo TCB wamejipanga kuhakikisha na kuona ndoto hizo zinatimia.
Dwashi amesisitiza kuwa,kuwa na ndoto pekee hakutoshi, bali kunahitajika hatua za makusudi na msaada sahihi ili kufikia mafanikio endelevu, huku akieleza kuwa hatua za watu binafsi katika kuboresha maisha yao huchochea pia fursa pana za kiuchumi katika jamii.
Katika kuimarisha utekelezaji wa kampeni hiyo,TCB Bank imeanza pia mpango wa kufufua akaunti zilizokuwa hazitumiki kwa muda mrefu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha uhusiano na wateja na kuboresha utoaji wa huduma.
Mbali na hilo, kampeni hiyo inatarajiwa kupanua wigo wa huduma kwa kujumuisha bidhaa za uwekezaji na bima, hatua inayolenga kuongeza ukaribu kati ya benki na wateja wake pamoja na kutoa suluhisho mahsusi kulingana na mahitaji yao.
Naye Meneja Mwandamizi wa TCB Bank, Al-Amin Lwano amesema,benki hiyo itawafikia moja kwa moja wajasiriamali katika maeneo yao ya biashara ili kuwapatia mikopo na huduma nyingine za kifedha zitakazosaidia kuongeza mtaji na kuboresha uzalishaji.
“Tutaenda karibu na wafanyabiashara ili kuwasaidia kukuza biashara zao na kuchochea uchumi wa nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa,uwezeshaji wa wananchi kupitia sekta ya fedha ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi endelevu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
TCB Bank imeeleza kuwa,mafanikio yake yanategemea mafanikio ya wateja wake, na kwamba itaendelea kushirikiana nao kwa karibu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa na maendeleo endelevu ya jamii kote nchini.
Tags
Benki ya Biashara Tanzania (TCB)
Benki ya TCB
Habari
I had a Dream
Lipa Popote na TCB
Nilikuwa na Ndoto
TCB Stawi Bond



























