NA DIRAMAKINI
MKUU wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt.Fredrick Shoo ametoa wito kwa Watanzania kuzingatia umuhimu wa upatanisho wa kweli na kusameheana ili kudumisha umoja na kusonga mbele kama taifa moja lenye mshikamano.
Akizungumza wakati wa ibada ya Pasaka iliyofanyika Usharika wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, Askofu Shoo amesema kuwa pamoja na uwepo wa hali ya utulivu na amani inayoonekana kwa sasa, bado mioyo ya watu wengi imebeba majeraha, chuki na maumivu yanayohitaji uponyaji wa kiroho kupitia neno la upatanisho.
Amesema,ni muhimu kwa Watanzania kuendelea kuiombea nchi ili kudumisha amani hiyo, akisisitiza kuwa upatanisho wa kweli huanzia moyoni kwa mtu binafsi.
“Tuendelee kuiombea sana nchi yetu katika kipindi hiki ambacho kunaonekana kuna utulivu na amani, lakini bado ndani ya mioyo ya watu wengi kuna mambo mazito. Tunamuomba Mungu aliyemfufua Kristo, Mungu wa upatanisho, aguse mioyo yetu ili tutafakari kwa kina neno la upatanisho,” amesema Askofu Shoo.
Ameeleza kuwa mfano wa Mungu kumtoa Yesu Kristo kwa ajili ya kuwapatanisha wanadamu na yeye unapaswa kuwa funzo kwa jamii, akibainisha kuwa unyenyekevu huo ni kielelezo tosha kwamba binadamu nao wanapaswa kuwa tayari kushuka na kusameheana.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa dini, hakuna uwezekano wa kujenga amani ya kudumu bila kuwepo kwa upatanisho wa kweli, unaojengwa juu ya ukweli, kuombana msamaha na kusameheana kwa dhati.
“Tutafute upatanisho kati yetu, pasipo upatanisho hakuna amani. Tunajua tulikopita kama taifa, na ili tuweze kusonga mbele tunahitaji kupatana. Upatanisho unakuja kwa kuambiana ukweli, kuombana msamaha na kusameheana,” amesisitiza.
Aidha, Askofu Shoo ameonya kuwa tabia ya kushupaza shingo na kukataa mazungumzo ni kikwazo kikubwa cha amani, akieleza kuwa hakuna changamoto isiyoweza kutatuliwa kupitia majadiliano ya dhati yanayozingatia unyenyekevu na utayari wa pande husika kufanya maridhiano.
Amewataka viongozi wa kisiasa, watawala na makundi mbalimbali ya kijamii kukaa pamoja na kujadili tofauti zao kwa lengo la kupata suluhu ya kudumu, akisisitiza kuwa mazungumzo ndiyo msingi mkuu wa kujenga taifa lenye mshikamano.
“Ni lazima pande zote zikubali kukaa pamoja na kuzungumza. Kila mmoja akishikilia msimamo wake na kukataa kushuka au kusikiliza wengine, hakutakuwa na mapatano wala amani ya kweli,” ameonya.
Katika wito wake kwa jamii, Askofu Shoo amewahimiza Watanzania kufungua mioyo yao pale walipokosana, kuombana msamaha na kusameheana, akisisitiza kuwa hakuna binadamu mkamilifu asiye na makosa.
Mbali na ngazi ya taifa, ameupanua wito huo hadi katika familia, akibainisha kuwa migogoro ya kifamilia inayosababisha mifarakano kati ya ndugu, wazazi, watoto na wanandoa ni chanzo cha maumivu makubwa kinachodhoofisha ustawi wa jamii kwa ujumla.
Sambamba na hayo, amewataka waumini kuendeleza maisha ya toba na mabadiliko ya kweli hata baada ya kumalizika kwa kipindi cha Kwaresma, akisisitiza kuwa maadhimisho ya Pasaka yanapaswa kuwa mwanzo wa maisha mapya yenye kumcha Mungu, badala ya kurejea katika mienendo ya awali isiyofaa.
Kwa ujumla, ujumbe wa Askofu Shoo umejikita katika kuhimiza mshikamano, maelewano na kujenga utamaduni wa kusameheana kama nguzo muhimu ya kudumisha amani na umoja wa kitaifa.
