NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, mchango wa hayati Sheikh Abeid Amani Karume katika kujenga taifa imara unaendelea kuwa dira kwa vizazi vya sasa na vijavyo huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya umoja, usawa na haki iliyoasisiwa na kiongozi huyo wa kihistoria.
"Leo tunaadhimisha Siku ya Kumbukizi ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na kiongozi shupavu aliyelijenga Taifa letu katika misingi ya usawa, umoja na haki.
"Tunaendelea kuuenzi mchango wake kwa kudumisha amani, mshikamano na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar na Taifa kwa ujumla. Mwenyezi Mungu amrehemu Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na kumpa pepo ya milele,"ameeleza Rais Dkt.Mwinyi.
Maadhimisho ya Siku ya Karume hufanyika kila mwaka Aprili 7, ikiwa ni kumbukizi ya kifo cha Sheikh Abeid Amani Karume, ambaye alitoa mchango mkubwa katika harakati za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na ujenzi wa taifa jipya lenye misingi ya usawa kwa wananchi wote.
