DAR-Katika hatua ya kuondoa changamoto za upatikanaji wa mitaji, hususan kwa biashara ndogo na za kati (MSMEs) pamoja na wauzaji wa bidhaa nje ya nchi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ipo katika mchakato wa kuanzisha kampuni ya usimamizi wa udhamini wa mikopo itakayojulikana kama Tanzania Credit Guarantee PLC.
Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC), kilichofanyika leo Aprili 20,2026 jijini Dar es Salaam, Naibu Gavana wa BoT, Bi. Sauda Kassim Msemo amesema kuwa, hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi, kuimarisha ubunifu na kuongeza wepesi katika utoaji wa huduma za dhamana ya mikopo nchini.
“Kwa zaidi ya miaka 20, mifuko ya dhamana ya mikopo ilisimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania. Sasa tunatenganisha majukumu ya usimamizi na utoaji dhamana ili kuondoa mgongano wa maslahi na kuongeza ufanisi wa utekelezaji,” amesema Bi. Msemo.
Ameongeza kuwa, kampuni hiyo itakuwa kichocheo muhimu cha utekelezaji wa nguzo tatu za Dira 2050 pamoja na vichocheo vitano vya mabadiliko ambavyo ni pamoja na usafirishaji jumuishi, nishati, sayansi na teknolojia, utafiti na maendeleo, pamoja na mabadiliko ya kidijitali.
Kupitia taasisi hiyo, uwekezaji katika sekta za uzalishaji kama kilimo, viwanda, uchumi wa buluu, huduma za kiteknolojia na biashara za kuuza bidhaa nje ya nchi utawezeshwa kwa kupunguza hatari za mikopo na hivyo kuvutia mitaji zaidi.
Bi. Msemo amewahimiza wadau wa sekta binafsi kutumia fursa hiyo kushiriki kikamilifu kama wabunifu na washirika wa maendeleo, akibainisha kuwa mfumo wa umiliki wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi utawezesha biashara za ndani kukua na kushindana kimataifa huku manufaa ya ukuaji yakiwafikia Watanzania wote.
Aidha, amesema mafanikio ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 yanategemea ushirikiano madhubuti kati ya sekta ya umma na binafsi, huku sekta binafsi ikipewa nafasi ya kuwa injini kuu ya ukuaji wa uchumi.
Ameongeza kuwa, Serikali imeweka msingi thabiti wa utekelezaji wa dira hiyo kwa kuhamasisha sekta zote kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi jumuishi, shindani na endelevu.




