DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuwa, Benki Kuu inaendelea kushirikiana kwa karibu na benki za biashara ili kuhakikisha viwango vya riba ya mikopo vinakua nafuu, huku ikiendelea kuheshimu misingi ya uchumi wa soko huria nchini.
Akizungumza kwa njia ya mtandao katika kikao na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), kilichofanyika leo Aprili 20,2026, Gavana Tutuba amesisitiza umuhimu wa uwazi katika utoaji wa taarifa za riba na gharama za huduma za kifedha kwa wananchi.
Ameeleza kuwa, Benki Kuu imeanza kutoa takwimu za kulinganisha ada na gharama zinazotozwa na benki pamoja na taasisi mbalimbali za fedha, hatua inayolenga kuwasaidia wateja kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
Kwa upande wa mifumo ya malipo, ameeleza kuwa, inaendelea kusimamiwa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha usalama, ufanisi na upatikanaji wake wakati wote.
Amesema kuwa,Mfumo wa Malipo ya Hapo kwa Papo (TIPS) unafanya kazi saa 24 kila siku na umeendelea kuwa salama na wa kuaminika, hivyo kuwawezesha wananchi kufanya miamala yao kwa urahisi wakati wowote.
Gavana Tutuba pia amesisitiza umuhimu wa kutumia mifumo ya kidijitali badala ya pesa taslimu, akieleza kuwa njia hizo ni salama, rahisi na zinaendana na maendeleo ya teknolojia.
Kuhusu upatikanaji wa fedha za kigeni, amefafanua kuwa, nchi hupata fedha hizo kupitia mauzo ya nje ya mazao ya kilimo na bidhaa mbalimbali, pamoja na sekta ya utalii na mikopo ya miradi ya maendeleo.
Amesisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kutumia mifumo rasmi kama benki na maduka ya kubadilisha fedha yaliyoidhinishwa na Benki Kuu wanapohitaji fedha za kigeni, na kubainisha kuwa ni kosa kufanya malipo ya ndani kwa kutumia fedha za kigeni.
Katika hatua nyingine, Gavana amebainisha kuwa,Benki Kuu kwa sasa inasimamia mifuko ya udhamini wa mikopo ambayo kufikia mwezi Julai,mwaka huu inatarajiwa kubadilishwa na kuwa kampuni inayojitegemea.
Kikao hicho kilitoa fursa kwa Jumuiya hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Bw. Severin Mushi, kuwasilisha maoni na changamoto zao, huku Benki Kuu ikiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuboresha mazingira ya biashara na huduma za kifedha nchini.



