Aliyekuwa Mhasibu wa KMC hatiani kwa makosa ya rushwa

NA DIRAMAKINI

APRILI 14,2026 Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ilimhukumu aliyekuwa Mhasibu wa Klabu ya Soka ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC FC),Bw.Atulinda Kyaruzi Barongo kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Shilingi milioni 3,000,000.
Ni baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka ya makosa ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.

Katika shauri la jinai namba ECo.13170/2025, mshtakiwa alifikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa matatu ambayo ni kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22.

Pia, ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28(1) pamoja na matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, toleo lililofanyiwa marejeo la mwaka 2022.

Ilidaiwa mahakamani kuwa, katika kipindi cha kati ya tarehe 1 hadi 4 Septemba 2020, mshtakiwa akiwa katika nafasi yake ya uhasibu ndani ya klabu hiyo, alitumia vibaya madaraka yake kwa kuandaa na kutumia nyaraka za uongo akionesha kuwa,kulikuwa na malipo yaliyofanyika kwa vibarua waliodaiwa kufanya kazi ya dharura katika Soko la Kawe.

Hata hivyo, uchunguzi ulibaini kuwa malipo hayo hayakufanyika kama ilivyowasilishwa, hatua iliyolenga kumdanganya mwajiri wake.

Aidha, upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa mshtakiwa alijihusisha na ubadhirifu wa fedha za umma alizokuwa amepewa dhamana ya kuzisimamia, jambo lililoisababishia Serikali hasara ya kifedha.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa katika makosa yote matatu yaliyokuwa yanamkabili.

Kufuatia hukumu hiyo, alipewa adhabu ya kifungo cha miaka miwili gerezani au kulipa faini ya Shilingi milioni tatu, ambapo alichagua kulipa faini hiyo.

Shauri hilo liliendeshwa na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Wilaya ya Kinondoni, Bi.Florida Mutalemwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here