Mlinzi jela miaka saba kwa kughushi nyaraka na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu

NA DIRAMAKINI

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imemhukumu kifungo cha miaka saba jela,Bw. Loti Joseph Fwalu baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kughushi nyaraka, kuwasilisha nyaraka za uongo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Hukumu hiyo imetolewa Aprili 16,2026 mbele ya Mheshimiwa Hakimu Amos Lweikiza katika shauri la Jinai Na.16365/2025 lililosikilizwa katika mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, mshtakiwa alikuwa mtumishi wa kampuni ya ulinzi ya Garda World, ambapo alitumia nafasi yake kutenda makosa hayo.

Ilidaiwa kuwa,mshitakiwa alitengeneza nyaraka za uongo zikiwemo barua ya kuachishwa kazi, hati ya huduma (certificate of service) pamoja na fomu ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ya kuomba mafao ya kuachishwa kazi.

Uchunguzi uliofanywa ulithibitisha kuwa, mshtakiwa hakuwahi kuachishwa kazi na mwajiri wake, lakini aliwasilisha nyaraka hizo kwa lengo la kujipatia fedha isivyo halali. Kupitia udanganyifu huo, alifanikiwa kujipatia jumla ya shilingi 3,873,221.

Mahakama iliridhika bila shaka yoyote kuwa, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha makosa dhidi ya mshtakiwa kwa mujibu wa vifungu vya 335, 337 na 305 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu [Sura ya 16, Marejeo ya 2022].

Akitoa hukumu, Mheshimiwa Hakimu Lweikiza alisisitiza umuhimu wa uadilifu mahali pa kazi na kuonya dhidi ya vitendo vya kughushi na udanganyifu vinavyoathiri taasisi na mifumo ya hifadhi ya jamii. Hivyo, alimhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka saba jela.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Bi.Janeth Kafuko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here