NA DIRAMAKINI
UJENZI wa bandari ya kisasa ya uvuvi ya Kilwa Masoko inayojengwa na kampuni ya Uhandisi wa Bandari ya China umefikia asilimia 97 ikiwa na gati lililokamilika lenye urefu wa mita 315 na jengo la kisasa ambalo limekamilika kwa asilimia 98.
Hatua hiyo inatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu pamoja na kukuza uchumi wa maeneo ya ukanda wa pwani.
Bandari hiyo, ambayo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya uvuvi nchini, inatarajiwa kuanza kutoa huduma mara baada ya kukamilika rasmi, huku serikali ikieleza kuwa mradi huo utaongeza uwezo wa Tanzania kuvua samaki katika maji ya kina kirefu na kuimarisha ushindani wa bidhaa za uvuvi katika soko la kimataifa.
Mamlaka husika zimeeleza kuwa, kukamilika kwa bandari hiyo kutasaidia kupunguza upotevu wa samaki baada ya mavuno, changamoto ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiathiri wavuvi wengi kutokana na ukosefu wa miundombinu bora ya uhifadhi, usafirishaji na usindikaji wa mazao ya baharini.
Aidha, mradi huo unatarajiwa kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi kupitia uwekezaji katika viwanda vya kuchakata samaki, uhifadhi wa baridi pamoja na mifumo ya kisasa ya usafirishaji wa bidhaa kwenda ndani na nje ya nchi.
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa, bandari hiyo inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Lindi na maeneo jirani kwa kuongeza ajira, mapato ya serikali pamoja na fursa za biashara kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli za uvuvi.
Mbali na kuimarisha sekta ya uvuvi, mradi huo pia unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za Tanzania za kukuza uchumi wa buluu kwa kutumia rasilimali za bahari kwa tija zaidi na kwa njia endelevu.

