ZANZIBAR-Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Abeida Rashid Abdallah amesema, Serikali ya Zanzibar inaendelea kuchukua juhudi mbalimbali za kuwalinda watoto dhidi ya aina zote za udhalilishaji na ukatili kupitia mifumo ya sheria rafiki kwa watoto, utoaji wa elimu kwa jamii pamoja na kuimarisha mifumo ya kuripoti na rufaa kwa waathirika.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu huyo, katika kikao cha wadau wa Mradi wa “PEACE” kilichofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Kibweni Unguja, Naibu Katibu wa Wizara hiyo, ndugu Khatib Mwadin Khatib Amesema juhudi hizo pia zinahusisha kuandaa mipango na mikakati maalum ya kuwalinda wanawake na watoto pamoja na kuimarisha mashirikiano baina ya taasisi mbalimbali.
Aidha,amesema licha ya jitihada hizo, bado vitendo vya udhalilishaji wa watoto vinaendelea kuwa changamoto kubwa nchini kwani matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto ya mwaka 2024 yameonesha kuwa asilimia 6 ya wanawake na wanaume Zanzibar wamepitia ukatili wa kingono, huku asilimia 9 ya wanawake na asilimia 20 ya wanaume wakikumbwa na ukatili wa kimwili.
Amesema,utafiti huo umebaini kuwa asilimia 11 ya wanawake na asilimia 19 ya wanaume wamepitia ukatili wa kihisia, hali ambayo imeongeza haja ya kuimarisha juhudi za kukabiliana na vitendo hivyo.
Pia,amesema kuwa udhalilishaji wa watoto hauhusishi watu wazima pekee bali pia hutokea baina ya watoto wenyewe na rika linalofanana. Afahamisha kwamba mazingira magumu yanayowakabili watoto yanachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo umaskini, ulemavu pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Ameeleza, mitandao ya kijamii, simu za mkononi na majukwaa ya mtandaoni yamefungua njia mpya za ukatili dhidi ya watoto na vijana, hivyo Serikali ina wajibu wa kuhakikisha watoto wanakuwa salama mtandaoni na nje ya mtandao.
Amefahamisha kwamba Mradi wa” PEACE” umefika kwa wakati muafaka kwani unalenga kuibua mbinu mpya za kushughulikia changamoto zinazowakabili watoto na vijana kwa kuwashirikisha vijana wenyewe kama sehemu ya suluhisho.
Amesema Mradi huo utasaidia kutoa taarifa za utafiti zitakazowezesha kuandaa programu maalum ya kupambana na ukatili wa kingono miongoni mwa watoto.
Mwisho amewashukuru wadau wa Maendeleo, taasisi ya YLabs na Gen ACT waliyoandaa kikao hicho kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kwa maslahi ya watoto, vijana na taifa kwa ujumla.
Naye Mshauri wa utafiti wa Mradi wa PEACE, Dkt. Samuel Likindikoki kutoka Chuo Kikuu Muhimbili amezungumzia kuhusu matokeo ya utafiti wa Kitaifa ya Ukatili na udhalilishaji dhidi Watoto na Vijana uliyofanyika mwaka 2024 (VACS 2024) ambayo ulionesha matokeo ya ngono kwa Watoto wa kike na kiume.
Amesema,matokeo hayo yameonesha Kitaifa asimilia tano (5%) Watoto wa kiume na 11 watoto wa kike wamefanyiwa ukatili wa ngono na kwa Zanzibar asilimia 6 ya watoto wa Kike na wakiume wamenyiwa ukatili wa kingono, lakini matokeo hayo hayasemi kama yalifanywa na wanarika (Watoto kwa Watoto).
Pia,amesema matokeo ya VACS 2024 yameonesha asilimia 95 ya wahanga hawajapatiwa huduma baada ya kufanyiwa ukatili/ udhalilishaji, hivyo utafiti wa PEACE utaangalia na kuja na hatua za kuongeza ufikiaji wa huduma hasa nafasi ya Jamii ili kusaidia kutokomeza udhalilishaji wa kingono kwa watoto na Vijana.
Kwa upande wa Taasisi ya Y. Labs akizungumza kiongozi wa Mradi huo, ndugu Willian Otuck amesema Mradi wa Peace ni Mradi wa Mwaka mmoja umeanza Febuari 2026 na utamaliza mwakani Januari 2027 ambapo Mradi unalengo la kufanya utafiti kuhusiana na Ngono kwa vijana kati ya Umri wa miaka 10- 24 na Unatekelezwa na taasisi ya YLabs kwa kushirikiana na Generation Action (GenAction) na unadhaminiwa na Oak Foundation na waterloo Foundation.









