NA MARY GWERA
Mahakama
JAJI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju ametoa wito kwa vijana wa Kitanzania waliopo katika fani mbalimbali kutumia vipaji vyao kuandika vitabu vitakavyotumika kwa manufaa ya Taifa.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akizindua Kitabu kiitwacho SING GRATITUDE kilichoandikwa na Wakili Msomi Aisha Saidi Kingu. Hafla ya uzinduzi wa Kitabu hicho imefanyika leo tarehe 10 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwandishi wa Kitabu hicho, Wakili Aisha Saidi Kingu.
Mhe. Masaju ameyasema hayo leo tarehe 10 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Kitabu kiitwacho SING GRATITUDE kilichoandikwa na Wakili Aisha Saidi Kingu.
“Vijana msisubiri mpaka muwe na kila kitu ili muweze kutumia vipaji vyenu, hivyo natoa wito kwa vijana wa Tanzania; kuandika, kusoma, kutafakari na kuchangia Taifa letu kwa vipaji vyenu. Taifa linalowapa vijana nafasi ya kuandika na kubuni hujenga urithi wa maarifa na mshikamano wa vizazi,” amesema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiteta jambo na Mwandishi wa Kitabu cha SING GRATITUDE, Wakili Aisha Saidi Kingu mara baada ya kukizindua kitabu hicho.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha SING GRATITUDE kilichoandikwa na Wakili Aisha Saidi Kingu (wa tatu kushoto).
Kadhalika, Mhe. Masaju ametoa rai kwa wananchi kuona wajibu wa kuunga mkono Waandishi wa Tanzania kwa kusoma kazi zao, kununua vitabu vyao, kuwapa mrejesho, kuwapa nafasi katika majukwaa ya mijadala na Vyombo vya Habari.
Akizungumzia kuhusu Kitabu hicho cha SING GRATITUDE ambacho amekizindua, Mhe. Masaju amempongeza Wakili Aisha kwa kukiandika na kusema kuwa, Kitabu hicho kina viwango na hadhi ya Kimataifa.
“Napenda kutumia fursa hii kumpongeza Wakili Aisha Saidi Kingu kwa ujasiri wa kuandika. Kuandika si kazi ndogo, inahitaji nidhamu, uvumilivu, kujitafakari na kukubali kubeba ujumbe ambao wengine wanaweza kuusoma, kuuchambua na kuuhoji. Ninampongeza pia kwa kuonesha kuwa kijana anaweza kuchangia ujenzi wa Taifa kwa njia nyingi. Mtu anaweza kuwa, Mwanasheria, Mshairi, Mwanadiplomasia, Msomaji na Mwandishi, kama alivyo Wakili Aisha,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesema kuwa, Vitabu vya fasihi vina nafasi kubwa sana katika maendeleo ya jamii kwa sababu husaidia kufundisha, kuelimisha na kuburudisha watu.
“Kwanza, vitabu vya fasihi hutoa elimu kwa jamii. Kupitia hadithi, riwaya, tamthilia na mashairi, watu hujifunza maadili mema kama vile uaminifu, heshima, uvumilivu na mshikamano. Fasihi pia huwafundisha watu kuhusu historia, mila na desturi za jamii mbalimbali, pili, fasihi huburudisha jamii. Wasomaji hupata furaha na kupunguza mawazo wanaposoma vitabu vya fasihi…,” ameeleza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kitabu kiitwacho SING GRATITUDE kilichoandaliwa na Wakili Aisha Saidi Kingu.
Ameeleza Kuandika vitabu vya fasihi ni jambo muhimu sana katika jamii kwa sababu huelimisha, huburudisha, hukemea maovu, huhifadhi utamaduni na kukuza lugha. Hivyo, jamii inapaswa kuwahamasisha waandishi wa fasihi ili waendelee kuandika vitabu vitakavyosaidia kujenga taifa lenye maadili mema na maendeleo.
Kuhusu umuhimu wa kuwa na Shukrani ambapo amesema kuwa, Jaji Mkuu amebainisha kuwa, ina faida lukuki kwa upande wa Kisaikolojia na Kimaisha, husaidia kupunguza msongo wa Mawazo, husaidia mtu kuona mema hata katika changamoto, na hivyo kupunguza wasiwasi na huzuni.
Mhe. Masaju amesema pia, shukrani huongeza furaha ya mtu binafsi, ambapo amesema, “Watu wanaoshukuru huishi maisha yenye matumaini na amani ya ndani.”
Ameongeza kuwa, manufaa mengine ya kuwa na Shukrani ni pamoja na kuimarisha afya ya akili ambapo Tafiti zinaonesha kuwa, shukrani hupunguza hisia za hasira na wivu na kuongeza kuridhika na maisha.
“Kwa upande wa Kijamii na Kiutamaduni, Shukrani huimarisha mshikamano wa kijamii: Jamii yenye shukrani hujenga uhusiano wa heshima na mshikamano, kwani watu wanapohisi kuthaminiwa, hujitolea zaidi kushirikiana, hujenga maadili ya uwajibikaji: Shukrani ni kiashiria cha kutambua mchango wa wengine, na hivyo kuimarisha utamaduni wa kuheshimiana na kusaidiana,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesema, Shukrani hujenga maadili ya uwajibikaji: Shukrani ni kiashiria cha kutambua mchango wa wengine, na hivyo kuimarisha utamaduni wa kuheshimiana na kusaidiana, uendeleza utamaduni wa amani.
Katika upande wa Kidini na Kiroho, Jaji Mkuu amesema, ni tendo la imani: Katika dini nyingi, shukrani ni ibada na ishara ya kutambua ukuu wa Mungu. Mfano, “Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu” (1 Wathesalonike 5:18).
“Shukrani huimarisha maadili ya kiroho, Shukrani hujenga moyo wa unyenyekevu na kutambua neema za Mungu katika maisha ya kila siku na kwa upande wa Kiuchumi na Kimaendeleo, huongeza tija kazini: Wafanyakazi wanaothaminiwa huonyesha bidii na uaminifu zaidi, huimarisha uongozi bora: Viongozi wanaoshukuru mchango wa wananchi hujenga imani na mshikamano wa kitaifa, huendeleza mshikamano wa kizazi kipya,” ameeleza.
Kwa upande mwingine, Mhe. Masaju amesema, kukosa shukrani kuna hatari kadhaa ikiwa ni pamoja na kujenga malalamiko na chuki, kupoteza mshikamano wa kijamii, kudhoofisha maadili ya kiroho na kitaifa:
“Kukosa shukrani ni ishara ya kutokubali uongozi wa Mungu na kupuuza mchango wa wengine. Shukrani si neno dogo bali ni nguzo ya maadili, mshikamano na maendeleo ya kijamii. Jamii inayojenga moyo wa shukrani huimarisha furaha ya watu wake, hujenga mshikamano wa kitaifa, na kuendeleza maadili ya uwajibikaji,” amesisitiza.
Akiwa katika mahojiano maalum wakati wa hafla hiyo, Mwandishi wa Kitabu cha SING GRATITUDE, Wakili Aisha amesema wazo la kuandika kitabu hicho lilianzia kwenye neno lisemalo ‘Muujiza upo katika asante’ (The Miracle is in the thank you).
Wakili Aisha amesema, njia kuu mojawapo ya shukrani ni kutambua na kuelewa uwepo wa sasa ambapo amesema, “kuchagua kushukuru kunakufanya usonge mbele, kushukuru kwenye udogo ndipo kuna ukubwa…..”
Picha za makundi mbalimbali ya wageni waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha SING GRATITUDE kilichoandikwa na Wakili Aisha Saidi Kingu.
Baba Mzazi wa Wakili Aisha Saidi Kingu, Dkt. Saidi Kingu Mtemi akizungumza wakati wa hafla hiyo. Kulia ni Mama Mzazi wa Wakili huyo.
Kiongozi wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Issa Issa akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha SING GRATITUDE kilichoandikwa na Wakili Aisha Saidi Kingu.
Padri Faustine Furaha akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha SING GRATITUDE kilichoandikwa na Wakili Aisha Saidi Kingu.Ameongeza kuwa, ana ndoto ya kuona vijana wanakuwa katika maadili mema ya Kitanzania, pamoja na kuendelea kuandika kuhusu masuala mbalimbali ya kuelimisha jamii ya Kitanzania.
Wakizungumzia umuhimu wa shukrani nao Viongozi wa Dini ya Kiislamu na Kikristo, Sheikh Issa Issa pamoja na Padri Faustine Furaha, kwa pamoja wamesema neno Shukrani limesisitizwa pia hata katika vitabu vya dini hizo. Mfano katika Biblia 1 Watheselonike 5:18 inasema; Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Na Katika Quran Tukufu- Surah Ibrahim 14:7 inasema, Mkinishukuru, hakika nitawazidishia.
“Tujenge utamaduni wa kumshukuru Mungu, Zaburi 136:1, nitamshukuru Bwana kwa ajili ya Haki yake na nitaliimbia.........Kwa muda mrefu sana dhana ya shukrani imepuuzwa, kuhesabu baraka huongeza nyingine,” amesema Padri Furaha.
Amesema, kushukuru ni kuangalia tulicho nacho na sio kile ambacho hatuna na kwamba shukrani ni tunda la uvumilivu na kwamba yatupasa kushukuru kabla ya kumuomba Mungu kwa kuwa moyo usiokuwa na shukrani hukausha mema yote.
Naye Sheikh Issa amesema, kushukuriwa na kupendwa ni miongoni mwa mahitaji ya binadamu.
Kwa upande wao Mchambuzi wa Kitabu, Bw. Joram Nkumbi pamoja na Mhariri wa Kitabu hicho, Dkt. Ishmail Mwambapa kwa pamoja wamempongeza Wakili Aisha na kusema kuwa, kitabu kilichoandikwa kwa mfumo wa mashairi kinaelimisha na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na shukrani katika hali yoyote katika maisha.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mwandishi wa Kitabu cha SING GRATITUDE, Wakili Aisha Saidi Kingu (kushoto) na kulia ni Mchambuzi wa Kitabu, Bw. Joram Nkumbi.
Mwandishi wa Kitabu cha SING GRATITUDE, Wakili Aisha Saidi Kingu (kushoto) akifanyiwa mahojiano kuhusu Kitabu hicho leo tarehe 10 Mei, 2026 wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho.(Picha na BAKARI MTAULLAH).
Bw. Nkumbi amesema, Kitabu kinaonyesha moyo wa Shukrani na kwamba muujiza mkubwa upo katika neno Asante, amesema “shukrani ni kama kuomba ten, ruhusu moyo wa shukrani uingie moyoni mwako, kitabu pia kinasisitiza mambo ya maadili.”
Katika kitabu hicho cha SING GRATITUDE kinamfundisha mtu kusema ahsante kwa mambo mema na makubwa, na pia kwa mambo madogo ambayo mara nyingi hupita bila kutambuliwa kirahisi.
Uzinduzi wa kitabu hicho ni ushahidi kuwa taifa letu lina hazina kubwa ya fikra na vipaji. Vijana kama Wakili Aisha wanapochukua kalamu na kuandika, wanajenga msingi wa leo na kesho yenye maarifa na matumaini.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu, Mabalozi, Wazazi pamoja na ndugu jamaa na marafiki wa familia ya Aisha Saidi Kingu.
















