Jela miaka 20 kwa kupatikana na meno ya tembo mkoani Mbeya

MBEYA-Mahakama ya Wilaya ya Mbarali imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela Frank Aron Mwakamalisya, mkazi wa Kijiji cha Igamba Wilaya ya Mbeya, baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria, ambazo ni meno nane ya tembo.
Hukumu hiyo imetolewa Mei 8, 2026 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Mhe. Nico Mwakibibi (SRM), baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa upande wa mashitaka uliweza kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote.

Awali, Mahakama ilielezwa kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 15, 2025, ambapo alikamatwa na askari wa Jeshi la Polisi katika eneo la Nsonyanga Wilaya ya Mbarali, akiwa na meno hayo ya tembo yenye thamani ya shilingi 198,044,800/=.

Upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Ruben Lubango uliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaojihusisha na vitendo vya ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali.

Akitoa hoja zake mbele ya Mahakama, Lubango alisisitiza kuwa,vitendo vya uwindaji haramu na biashara ya nyara za wanyamapori vinaendelea kuhatarisha uhifadhi wa rasilimali za taifa pamoja na kuathiri juhudi za Serikali katika kulinda bioanuwai na utalii.

Mahakama ilikubaliana na hoja za upande wa mashitaka na kutoa adhabu hiyo kali kwa lengo la kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa wanyamapori na kulinda rasilimali za asili za nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here