NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni jijini Dar es Salaam imemhukumu mfanyabiashara, Aliasgher Akhter Khakoo kifungo cha miaka miwili gerezani au kulipa faini ya Shilingi milioni 3,000,000, pamoja na kurejesha kiasi cha Shilingi milioni 60,000,000 alichojipatia kwa njia ya udanganyifu.
Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 29, 2026 katika shauri la jinai namba 15378/2025, ambapo mshtakiwa alikabiliwa na shtaka la kuwasilisha hundi benki kwa lengo la kupata fedha ilhali akifahamu kuwa akaunti yake haikuwa na fedha za kutosha. Kitendo hicho kinajulikana kisheria kama “kurusha kishada” (kite flying).
Kwa mujibu wa mashtaka, kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 332B(1) na (3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2022. Mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Baada ya kutiwa hatiani, mshtakiwa alichagua kulipa faini ya Shilingi milioni 3,000,000 badala ya kutumikia kifungo cha gerezani, kama ilivyoainishwa kwenye hukumu hiyo. Aidha, aliamriwa kurejesha kiasi cha fedha alichopata kwa njia hiyo isiyo halali.
Shauri hili liliendeshwa na waendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kinondoni ambao ni Bw. Aidan Samali na Bi. Stella Mwengwa.
.jpeg)