NA DIRAMAKINI
RAIS wa Marekani, Donald J. Trump amesema, utawala wake umeimarisha usalama wa taifa hilo kupitia operesheni kali dhidi ya ugaidi, magenge ya kihalifu na mitandao ya usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, huku akisisitiza kuwa Marekani imerejea katika nafasi yake ya nguvu duniani.
Rais wa Marekani, Donald Trump.(Picha na Anna Moneymaker/Getty Images).
Katika utangulizi maalumu wa mkakati mpya wa kupambana na ugaidi uliotolewa Mei 2026 akiwa Ikulu ya White House, Trump amesema, kurejea kwake madarakani Januari 20, 2025 kulihitimisha kile alichokiita “kipindi cha udhaifu, kushindwa na fedheha” chini ya utawala uliopita.
Amesema,kwa sasa Marekani imeimarisha ulinzi wa mipaka yake, kurejesha heshima yake kimataifa na kuweka mbele maslahi ya taifa hilo kupitia sera ya “America First”.
Katika maelezo yake, Trump amesema serikali yake imeongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa na wa ndani, akibainisha kuwa ndani ya siku 43 tangu kuingia madarakani, vikosi vya usalama vya Marekani vilifanikiwa kumkamata kinara aliyedaiwa kupanga shambulio la Abbey Gate nchini Afghanistan lililosababisha vifo vya wanajeshi 13 wa Marekani.
Aidha, ameeleza kuwa,katika kipindi cha mwaka mmoja, Marekani ilifanikiwa kuwaokoa mateka 106 wa Marekani waliokuwa wanashikiliwa nje ya nchi bila kulipa fedha yoyote kwa watekaji wao.
Trump pia amesema,baadhi ya matawi ya kundi la Muslim Brotherhood yalitangazwa rasmi kuwa mashirika ya kigaidi, hatua aliyodai inalenga kudhibiti misimamo mikali na vitendo vya kigaidi duniani.
Rais huyo amesema,Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani imepewa jukumu maalumu la kuwaondoa wahamiaji haramu wenye rekodi za uhalifu pamoja na watu wanaoshukiwa kuunga mkono itikadi kali za kijihadi.
Kwa mujibu wa Trump, hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kuzuia Marekani kuwa maficho ya wahalifu au watu wenye misimamo ya kigaidi.
Katika taarifa hiyo, Trump pia amezungumzia mgogoro wa Mashariki ya Kati akisema serikali yake ilichangia kusitishwa kwa vita vya Gaza, kuachiliwa kwa mateka waliokuwa wamebaki, pamoja na kuanzisha mchakato wa kuhakikisha eneo hilo halitumiki tena kama kitovu cha ugaidi na misimamo mikali.
Amedai kuwa operesheni za kijeshi zilizopewa majina ya “Midnight Hammer” na “Epic Fury” zilitoa pigo kubwa dhidi ya Iran, taifa alilolitaja kuwa mfadhili mkuu wa ugaidi duniani.
Trump amesema,serikali yake imeweka mkazo mkubwa katika kuvunja nguvu za magenge ya dawa za kulevya na uhalifu wa kupangwa katika ukanda wa Amerika.
Amevituhumu vikundi hivyo kwa kusababisha vifo vya mamilioni ya wananchi wa Marekani kupitia dawa za kulevya, biashara haramu ya silaha pamoja na usafirishaji wa wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa rais huyo, baadhi ya magenge hayo yalitangazwa rasmi kuwa mashirika ya kigaidi, huku jeshi la Marekani likipewa mamlaka ya kutumia nguvu kuyadhibiti na kuyasambaratisha.
Trump pia amedai kuwa,vikosi vya Marekani vilifanikiwa kumkamata kiongozi wa Venezuela, Nicolás Maduro kwa madai ya kuhusika na ugaidi wa dawa za kulevya, hatua ambayo amesema ilikuwa sehemu ya kuimarisha sheria na haki.
Akihitimisha ujumbe wake, Trump amesema mkakati mpya wa Marekani dhidi ya ugaidi unalenga kurejesha kile alichokiita “amani kupitia nguvu”, akionya kuwa Marekani haitavumilia mashambulizi dhidi ya raia wake.
“Ukidhuru Wamarekani au unapanga kuwadhuru, tutakutafuta na tutakuangamiza,” amesema Trump katika kauli yenye kuashiria msimamo mkali wa kiusalama wa utawala wake.
Tamko hilo linaendelea kuzua mijadala kimataifa kuhusu athari zake kwa diplomasia, usalama wa kimataifa na haki za binadamu, huku wachambuzi wakitathmini namna sera hizo zitakavyoathiri mahusiano ya Marekani na mataifa mengine duniani.

