Reli ya kisasa yaongeza kasi ya uchumi Tanzania,Profesa Mbarawa aweka wazi mafanikio ya TRC bungeni

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Uchukuzi imesema, itaendelea kuimarisha sekta ya usafiri wa reli nchini kwa kuendeleza ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), kuboresha reli ya zamani ya Meter Gauge Railway (MGR), pamoja na kufufua Reli ya TAZARA ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Hayo yameelezwa leo Mei 13,2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Katika hatua inayotajwa kuwa mafanikio makubwa ya mageuzi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), Serikali imetangaza kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 shirika hilo halitapatiwa tena ruzuku ya mishahara kutoka serikalini.

Profesa Mbarawa amesema,hatua hiyo ni matokeo ya maboresho yaliyoanza mwaka 2017, ambapo Serikali imekuwa ikiwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya reli,ununuzi wa vifaa na kuimarisha huduma za usafiri wa reli nchini.

Amesema,mageuzi hayo yameiwezesha TRC kuongeza uwezo wa kiutendaji na kuanza kujitegemea kifedha hatua kwa hatua.
Pia,Waziri Mbarawa amesema,Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa reli ya SGR pamoja na maboresho ya reli ya MGR yenye urefu wa takriban kilomita 2,707.

Amefafanua kuwa,mradi wa SGR unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza inahusisha kilomita 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, huku awamu ya pili ikijumuisha kilomita 1,590 kutoka Tabora hadi Kigoma pamoja na kipande cha Uvinza-Musongati.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kukamilika kwa awamu hizo kutafanya Tanzania kuwa na jumla ya kilomita 2,809 za reli ya kisasa ya SGR.

Ameeleza kuwa,hadi Machi 2026, ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam–Morogoro chenye kilomita 300 pamoja na kipande cha Morogoro–Makutupora chenye kilomita 422 ulikuwa umekamilika kwa kiwango kikubwa na huduma za treni tayari zinaendelea kutolewa katika maeneo hayo.
Aidha, amesema ujenzi wa kipande cha Mwanza–Isaka chenye kilomita 341 umefikia asilimia 68.77.

Profesa Mbarawa amesema,Serikali imepata suluhisho la changamoto zilizokuwa zikikwamisha kasi ya ujenzi wa vipande vya Makutupora–Tabora na Tabora–Isaka.

Amesema,Serikali imefanikiwa kupata mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani bilioni 1.277, sawa na takriban Shilingi trilioni 3.32, kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vipande hivyo viwili.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, fedha hizo zinatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo muhimu wa kimkakati kwa uchumi wa taifa.

Wakati huo huo,Serikali imeeleza kuwa, huduma za usafiri wa abiria kupitia reli ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma zimeendelea kuimarika.

Profesa Mbarawa amesema, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya abiria milioni 2.51 walitumia huduma hiyo ikilinganishwa na abiria milioni 2.05 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema,ongezeko hilo ni sawa na asilimia 22.40, hali inaoonesha kuongezeka kwa imani ya wananchi katika usafiri wa reli ya kisasa.

Kwa upande wa usafirishaji wa mizigo, Waziri huyo amesema, TRC ilisafirisha tani 102,452 za mizigo kupitia reli ya SGR katika kipindi hicho, ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuhamasisha matumizi ya reli katika usafirishaji wa mizigo.

Katika jitihada za kuongeza ufanisi wa usafirishaji, Serikali imeendelea na uunganishaji wa reli za SGR na MGR katika eneo la Ruvu.

Waziri Mbarawa amesema,utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 85 na unalenga kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Tanga.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kuunganisha reli hizo katika eneo la Bahi kwa ajili ya kuwezesha uhamishaji wa mizigo kati ya reli hizo mbili.

Katika kuboresha reli ya MGR, Serikali imeendelea kubadilisha reli nyepesi kwa kuweka reli nzito pamoja na kuongeza uwezo wa madaraja kupitia Mfuko wa Reli.

Profesa Mbarawa amesema, hadi Machi 2026, ukarabati wa kipande cha Kaliua–Mpanda ulikuwa umefikia asilimia 32.72.

Aidha, Serikali imekamilisha karibu asilimia 99 ya ujenzi wa njia mpya ya reli yenye urefu wa kilomita 6.2 pamoja na daraja katika eneo la Godegode–Gulwe kwa ajili ya kukabiliana na mafuriko yaliyokuwa yakiathiri usafiri wa reli katika eneo la Kilosa–Kidete–Igandu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali pia inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa mabwawa sita katika Mto Kinyasungwe kupitia Mradi wa TIRP II ili kupunguza mafuriko na kuhakikisha reli zinafanya kazi kwa mwaka mzima bila usumbufu.

Vilevile,Waziri Mbarawa amesema, Serikali za Tanzania na Zambia zimeendelea kushirikiana katika kuboresha huduma za Reli ya TAZARA ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto za uchakavu wa miundombinu na uhaba wa vitendea kazi.

Amesema,kufuatia maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyotolewa wakati wa ufunguzi wa Bunge la 13 mwezi Novemba 2025, Serikali mbili zilianza rasmi mkakati wa kufufua reli hiyo.
Profesa Mbarawa amesema,mradi wa ufufuaji wa TAZARA ulizinduliwa rasmi Novemba 20, 2025 mjini Lusaka, Zambia, baada ya Tanzania na Zambia kusaini mkataba wa uendeshaji na Kampuni ya CCECC.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kampuni hiyo itawekeza dola za Marekani bilioni 1.4, sawa na takriban Shilingi trilioni 3.6, kwa ajili ya maboresho ya reli hiyo.

Amesema,maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa kusafirisha mizigo kufikia tani milioni 2.4 kwa mwaka pamoja na kuzalisha ajira mpya 100,000.

TRC yapongezwa

Mbali na hayo,Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Wizara ya Uchukuzi pamoja na uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa mafanikio ya shirika hilo kuanza kujitegemea katika kugharamia mishahara ya watumishi wake kupitia mapato ya ndani, hatua inayotajwa kuwa ishara ya kuimarika kwa sekta ya reli nchini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso ametoa pongezi hizo wakati akiwasilisha taarifa ya kamati kuhusu uchambuzi wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 Bungeni mjini Dodoma.

Amesema Serikali kwa kiwango kikubwa imezingatia maoni na ushauri uliotolewa na kamati hiyo wakati wa kujadili bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2025/2026, huku moja ya mafanikio makubwa ikiwa ni hatua ya Shirika la Reli Tanzania kuanza kuchangia mishahara ya watumishi wake kwa kutumia mapato ya ndani bila kutegemea ruzuku ya Serikali.
Kakoso amesema,  hatua hiyo ni matokeo ya usimamizi madhubuti unaofanywa na Wizara ya Uchukuzi chini ya Waziri Makame Mbarawa pamoja na uongozi wa TRC unaoongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Masanja Machibya.

“Kamati inaipongeza Wizara ya Uchukuzi chini ya Waziri Profesa Makame Mbarawa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Machibya kwa usimamizi madhubuti hadi kufikia hatua hiyo."

Amesema,mafanikio hayo yanaashiria kuimarika kwa utendaji wa shirika hilo pamoja na kuongeza uwezo wa sekta ya reli kujiendesha kwa ufanisi kupitia mapato yake yenyewe.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Aboubakar Asenga amepongeza juhudi za uongozi wa TRC katika usimamizi wa mradi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), akisema huduma ya treni kati ya Dar es Salaam na Dodoma imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri nchini.

Amesema,Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Masanja Machibya, ni miongoni mwa wataalamu vijana waliobobea katika taaluma ya reli na ameonyesha uwezo mkubwa katika kusimamia miradi ya kimkakati ya taifa.

“Huko Shirika la Reli Tanzania yupo kijana anaitwa Mhandisi Masanja Machibya, ni mhandisi ambaye amesomea reli, ameaminiwa na Rais Samia na pia Watanzania wamemuamini. Anafanya kazi kubwa na mafanikio tumepata."

Mbunge huyo amesema wananchi wengi wameendelea kunufaika na huduma ya treni ya SGR kutokana na kuimarika kwa usalama, kasi na ufanisi wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma, hali ambayo imeongeza imani ya wananchi kwa usafiri wa reli.

Ameitaka Serikali kuhakikisha inatafuta fedha kwa wakati kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa reli hiyo kuelekea mikoa ya Mwanza na Kigoma ili kuongeza mchango wa sekta ya reli katika uchumi wa taifa.

Wizara yaomba Bajeti ya Trilioni 2.87

Katika mwaka wa fedha 2026/27, Wizara ya Uchukuzi imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 2.87 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 126.04 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Shilingi trilioni 2.74 zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan katika sekta ya reli, bandari na usafiri wa anga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here