DCEA yafichua mbinu mpya za wahalifu wa dawa za kulevya,yasema iwe mchana au usiku hakuna atakayesalimika

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukamata jumla ya lita 66,048 za kemikali bashirifu zilizoingizwa nchini kinyume cha taratibu za kisheria katika operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Aprili,mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 13, 2026 katika ofisi za mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema,operesheni hiyo ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali za kudhibiti matumizi haramu ya kemikali zinazoweza kutumika katika utengenezaji wa dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa Kamishna Lyimo, kemikali zilizokamatwa ni pamoja na lita 16,048 za kemikali aina ya Cyclohexanone pamoja na lita 50,000 za Extra Neutral Alcohol (ENA).
Aidha, magari mawili yaliyotumika kusafirisha kemikali hizo yameshikiliwa huku watuhumiwa wawili wakikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Kamisha Jenerali Lyimo amesema,kutokana na kuimarika kwa mifumo ya udhibiti wa dawa za kulevya duniani, mitandao ya kihalifu imekuwa ikibadili mbinu kwa kutumia kemikali bashirifu kuzalisha dawa za kulevya katika maabara bubu.

Amefafanua kuwa,kemikali hizo hutumika kihalali katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, tiba, kilimo, ujenzi,madini na tafiti za kisayansi, lakini baadhi ya wahalifu huzitumia vibaya kwa kuzichepusha kutoka katika matumizi halali na kuzitumia kutengeneza dawa za kulevya.

“Hali hii imeongeza changamoto katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya duniani na kuifanya Tanzania kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa kemikali bashirifu ili kuzuia uchepushwaji wake katika matumizi haramu,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na mamlaka husika umebaini kuwa,kemikali aina ya Cyclohexanone ziliingizwa nchini na kampuni ya Kinglion Investment Company Limited bila kuzingatia matakwa ya sheria na taratibu za udhibiti, ikiwemo kukosa vibali kutoka mamlaka zinazohusika.
Aidha, imebainika kuwa kemikali aina ya Extra Neutral Alcohol (ENA) zilikuwa zikisafirishwa kwa kutumia magari yanayotumika kubeba mafuta ya petroli, yaliyoandikwa “Danger Petroleum 3YE 1203” aina ya Scania, huku vibali vilivyotumika vikidaiwa kuwa vya kughushi.

Magari hayo yalikuwa yakibeba kemikali kutoka kampuni ya Maranile Group Company Limited iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

Katika operesheni hiyo, DCEA imemkamata Bakira Abel Zacharia (44) mkazi wa Dar es Salaam na dereva wa gari lenye namba T 794 BMB pamoja na tela tenki namba T 166 AHW, lililokuwa limebeba lita 30,000 za kemikali hizo.

Mtu mwingine aliyekamatwa ni Vicent Stephen Rashid (26) mkazi wa Mbeya ambaye alikuwa dereva wa gari namba T 568 EQF lenye tela tenki namba T 640 EQN lililokuwa limebeba lita 20,000 za kemikali hizo.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema,mazingira ya uingizaji na usafirishaji wa kemikali hizo yanaashiria uwepo wa nia ovu ya kuzichepusha kwa matumizi haramu, hususan katika utengenezaji wa dawa za kulevya.

Ameeleza kuwa,kemikali aina ya Cyclohexanone ni miongoni mwa kemikali zinazotajwa katika taarifa mbalimbali za kimataifa kuwa hutumika katika maabara haramu zinazozalisha dawa za kulevya aina ya Phencyclidine (PCP).
Kwa mujibu wa DCEA, lita 16,048 za Cyclohexanone zilizokamatwa zingeweza kuzalisha takribani tani 11.4 za dawa za kulevya aina ya PCP iwapo zingefanikiwa kuchezushwa kwa matumizi haramu, kutokana na uwezo wa kilo moja ya kemikali hiyo kuzalisha wastani wa gramu 750 za dawa hizo.

Akizungumzia upande wa sheria, Kamishna Lyimo amesema,Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, Sura ya 182 inaelekeza kuwa, usafirishaji wa kemikali unapaswa kufanyika kwa kufuata taratibu maalumu, ikiwemo upatikanaji wa vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali husika.

Ameongeza kuwa,matumizi ya vibali vya kughushi pamoja na utoaji wa taarifa za uongo kuhusu matumizi yaliyokusudiwa ya kemikali ni kosa la jinai linalochukuliwa kwa uzito mkubwa na mamlaka za usimamizi.

Vilevile, amesema matumizi ya magari ya kubeba mafuta ya petroli katika kusafirisha kemikali hizo kwa njia fiche ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu za usalama na udhibiti wa kemikali, hali inayodhihirisha uwepo wa jaribio la kuzichepusha kwa matumizi haramu.

Katika hatua nyingine, DCEA imeeleza kuwa sambamba na operesheni hiyo, ilifanya operesheni nyingine katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, Njombe, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza ambapo jumla ya tani 5.733 za bangi, tani 1.67 za mirungi, gramu 48.23 za heroini pamoja na gramu 113.35 za cocaine zilikamatwa.
Aidha, ekari 38.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa, huku magari manne na pikipiki 14 zilizokuwa zikihusishwa na biashara hiyo haramu zikikamatwa. Jumla ya watuhumiwa 84 walitiwa mbaroni kuhusiana na operesheni hizo.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema,DCEA itaendelea kushirikiana na taasisi za kitaifa na kimataifa katika kuimarisha udhibiti wa kemikali bashirifu zinazoweza kutumika kuzalisha dawa za kulevya.

Pia ametoa wito kwa wadau wa sekta ya kemikali nchini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa pamoja na kushirikiana na vyombo vya usimamizi ili kulinda usalama wa jamii na uchumi wa taifa.

“Hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uchepushaji wa kemikali pamoja na biashara ya dawa za kulevya,”amesisitiza.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kuhusu vitendo vinavyohusiana na dawa za kulevya na uchepushaji wa kemikali bashirifu ili kusaidia juhudi za Serikali katika kupambana na biashara hiyo haramu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here