KAGERA-Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi,ACP Mimata tarehe 4 Mei,2026 ametoa elimu kwa wamiliki na wasimamizi wa Kampuni Binafsi za Ulinzi kuhusu njia bora za kuajiri walinzi wenye sifa na tabia njema ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji ndani na nje ya kampuni hizo.
ACP Mimata ameyasema hayo katika ukumbi wa Polisi Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, kufuatia kubaini kuwapo kwa upungufu wa umakini katika utekelezaji wa majukumu ya kiulinzi kwa baadhi ya kampuni.
Katika kikao hicho, pia alieleza utaratibu sahihi wa upatikanaji wa silaha kwa kampuni binafsi ya ulinzi, akisisitiza umuhimu wa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Aidha, alitoa maelekezo ya namna ya kushughulikia silaha zilizohifadhiwa katika vituo vya Polisi, hususan kabla ya kupata vibali rasmi kutoka serikalini.
Vilevile, ACP Mimata amewahimiza wamiliki na wasimamizi wa kampuni hizo kupunguza migogoro baina yao na kuimarisha ushirikiano, hatua itakayosaidia kukabiliana na changamoto zinazowakumba, ikiwemo mienendo isiyofaa ya baadhi ya walinzi wanapokiuka taratibu za kazi.
Amesisitiza kuwa,nidhamu, maadili na ushirikiano ni msingi muhimu katika kuboresha huduma za ulinzi na kuimarisha usalama wa jamii kwa ujumla.
