NA DIRAMAKINI
ALIYEKUWA Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kibaoni,Daniel Mwaniloli Richard na Vicent Zacharia Manyanza ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni katika Kata ya Kibaoni Wilaya ya Mlele mkoani Katavi wametiwa hatiani kaa makosa ya uhujumu uchumi.
Hukumu yao imetolewa Juni 26,2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Mlele iliyopo Inyonga, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mheshimiwa Andrea Njau.
Ni katika Shauri la Uhujumu Uchumi Na.ECC 16150/2026 kati ya Jamhuri dhidi ya Daniel Mwaniloli Richard na Vicent Zacharia Manyanza.
Washtakiwa hao walitiwa hatiani kwa kosa la ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma kiasi cha shilingi 3,810,000 walichokipata kwa kutumia vibaya madaraka yao.
Fedha hizo zilijumuisha shilingi 2,300,000 zilizotolewa na Zakaria Robert Mbogo ili apatiwe eneo la Serikali ya Kijiji baada ya kupisha eneo lake kwa ajili ya ujenzi wa barabara, pamoja na shilingi 1,510,000 zilizotolewa na Medard Nicodem Rajabu kwa madhumuni hayo hayo.
Badala ya fedha hizo kuingizwa katika akaunti ya Serikali ya Kijiji, washtakiwa walizitumia fedha hizo kwa manufaa yao binafsi na kuisababishia Serikali ya Kijiji cha Kibaoni hasara ya shilingi 3,810,000.
Washtakiwa walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya 2023, kikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Uhalifu wa Kupangwa (Economic and Organised Crime Control Act), Sura ya 200, Marejeo ya 2022.
Shauri hilo liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Msomi John Kitutu.
Kabla ya hukumu kutolewa, washtakiwa walifanya makubaliano ya kukiri kosa (Plea Bargaining Agreement) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Mahakama iliwatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu kutumikia kifungo cha nje cha miezi 12. Aidha, Mahakama iliamuru warejeshe fedha zote walizofanyia ubadhirifu kiasi cha shilingi 3,810,000 kwa Serikali ya Kijiji cha Kibaoni.
Hadi hukumu inatolewa, washtakiwa walikuwa tayari wamerejesha fedha zote kiasi cha shilingi 3,810,000 katika akaunti ya Serikali ya Kijiji cha Kibaoni iliyopo CRDB Bank.
