NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imemtia hatiani Mtendaji wa Kijiji cha Kigadye kilichopo Kata ya Heru Ushingo, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Elias Kazili Bakimbaga (54) baada ya kupatikana na hatia ya kuomba na kupokea rushwa.

Hukumu hiyo imetolewa Juni 25,2026 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kasulu, Mheshimiwa S.A. Mchalo katika shauri la jinai namba CC.11343/2026, la Jamhuri dhidi ya Elias Kazili Bakimbaga.
Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), James Mosi Nyarobi na Davis Junior.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Bakimbaga alishtakiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa, kinyume na Kifungu cha 15(1)(a) na 15(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA), Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2023.
Mahakama ilielezwa kuwa,Machi 21,2025 mtuhumiwa alimuomba Bi.Helena Juma fedha kiasi cha shilingi 150,000 ili amwachie huru mume wake, Mashilimu Kinasa ambaye alikuwa ameshikiliwa katika ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Kigadye kwa tuhuma za kuingia na kulima shamba la mtu mwingine bila ridhaa ya mmiliki.
Ilidaiwa kuwa,Januari 23, 2026, Bakimbaga alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Helena Juma, bila kufahamu kuwa fedha hizo zilikuwa zimeandaliwa na maafisa wa TAKUKURU Kasulu katika operesheni maalumu ya mtego wa rushwa.
Baada ya kupokea fedha hizo, maafisa wa TAKUKURU walimkamata mtuhumiwa papo hapo na kuanzisha hatua za kisheria zilizofikisha shauri hilo mahakamani.
Baada ya kusikiliza ushahidi na hoja zilizowasilishwa na upande wa mashtaka, Mahakama ilimpata mshtakiwa na hatia na kuamuru alipe fidia kwa Serikali ya shilingi 300,000 pamoja na faini ya mahakama ya shilingi 200,000.