BoT yasisitiza elimu ya fedha kuongeza ujumuishaji wa kifedha kote nchini

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha elimu ya fedha nchini ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya huduma rasmi za kifedha, uwekezaji na fursa za kiuchumi, hatua inayolenga kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.
Hayo yamesemwa leo Juni 29,2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anayesimamia Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo wakati akifungua Jukwaa la Elimu ya Fedha 2026 lenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha kwa Maendeleo Yetu Sote."

Akizungumza mbele ya wawakilishi wa taasisi za kifedha, wakufunzi wa elimu ya fedha, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na viongozi mbalimbali, Bi.Msemo amesema,jukwaa hilo ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata elimu ya fedha na kushiriki kikamilifu katika mfumo rasmi wa huduma za kifedha.

Aidha, akiwasilisha pia salamu za Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania,Emmanuel Tutuba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Fedha Jumuishi nchini amesema,baraza hilo limeendelea kuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kusogeza mbele ajenda ya ujumuishaji wa kifedha.

Bi.Msemo amesema,Jukwaa la Elimu ya Fedha limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Fedha Zanzibar, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wadhibiti wa sekta ya fedha, benki, taasisi za fedha pamoja na wakufunzi wa elimu ya fedha.

Amesema, lengo kuu ni kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia watoto, vijana na watu wazima, wakiwemo wale ambao hawapo katika mfumo rasmi wa elimu ili kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya fedha,akiba na uwekezaji.

“Tumekutana hapa kutathmini hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuhakikisha elimu ya fedha inakuwa sehemu ya utaratibu endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho. Ushirikiano wa wadau wote umeendelea kuleta matokeo chanya katika kuongeza matumizi ya huduma rasmi za kifedha nchini,”amesema.

Kwa mujibu wa Naibu Gavana Msemo, utafiti wa mwaka 2023 unaonesha kiwango cha ujumuishaji wa kifedha nchini kilifikia asilimia 76, mafanikio ambayo kwa kiasi kikubwa yalichochewa na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kifedha kidijitali.

Hata hivyo, amesema utafiti huo pia ulionesha kuwa bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kuhusu fursa za uwekezaji na matumizi sahihi ya bidhaa na huduma mbalimbali za kifedha.

Ameeleza kuwa, juhudi zinazoendelea za kutoa elimu ya fedha zimeanza kuzaa matunda, huku wananchi wengi zaidi wakionesha uelewa kuhusu umuhimu wa kutumia huduma rasmi za kifedha na kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi.

“Tunatarajia tathmini zijazo zitaonesha ongezeko la wananchi wanaotumia huduma za benki, bima, mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na soko la mitaji kutokana na elimu inayoendelea kutolewa,”amesema Bi.Msemo.

Naibu Gavana huyo amewataka wadau wa sekta ya fedha kuendelea kubuni mbinu bunifu za kufikisha elimu hiyo kwa wananchi wengi zaidi, ili kuongeza matumizi ya huduma rasmi za kifedha katika maeneo yote ya nchi.

Amesema,Serikali kupitia Wizara ya Fedha inaendelea kutekeleza Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2021 hadi 2029/30, ambao umetenga nafasi muhimu ya kuimarisha elimu ya fedha nchini.

Aidha, amesema Benki Kuu kupitia Baraza la Taifa la Fedha Jumuishi imeendelea kutekeleza Mkakati wa Tatu wa Huduma Jumuishi za Kifedha ulioanza mwaka 2023 na unaotarajiwa kukamilika mwaka 2028, ambapo elimu ya fedha ni moja ya maeneo ya kipaumbele.

Msemo amesema,ushirikiano kati ya Baraza la Taifa la Fedha Jumuishi na wadau mbalimbali umechangia kuongezeka kwa idadi ya wakufunzi wa elimu ya fedha wanaohudumia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amebainisha kuwa,hadi kufikia Juni mwaka huu, jumla ya wakufunzi 1,670 wameidhinishwa rasmi kutoa elimu ya fedha, huku taasisi 14 za elimu zikiendelea kutoa mafunzo ya kuwaandaa wakufunzi hao.

Pia, ameongeza kuwa,mafanikio hayo yamewezekana kutokana na ushirikiano mkubwa wa taasisi za elimu pamoja na watoa huduma za kifedha ambao wameendelea kuwekeza katika programu mbalimbali za elimu ya fedha kwa makundi tofauti ya wananchi.

Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Watoa Elimu ya Kifedha Waliothibitishwa nchini, Mark Peter amesema,taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi katika maeneo ya mijini na vijijini ili waweze kutumia kikamilifu fursa zinazopatikana katika sekta ya fedha na kuchangia maendeleo yao na uchumi wa nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here