NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imezindua rasmi filamu maalumu ya elimu ijulikanayo kama “Kifurushi” yenye lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mbinu zinazotumiwa kusafirisha dawa za kulevya kupitia vyombo vya usafiri wa umma na kuwatahadharisha wananchi dhidi ya kubeba mizigo au vifurushi wasivyovifahamu.
Uzinduzi huo umefanyika Juni 12, 2026 katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji, wasanii,waigizaji na taasisi zinazoshiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema,dawa za kulevya zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya za wananchi, ustawi wa familia, usalama wa jamii na maendeleo ya taifa kutokana na madhara yake makubwa ya kijamii na kiuchumi.
Amesema,matumizi na biashara ya dawa za kulevya huchangia kuongezeka kwa uhalifu, kuvunjika kwa familia, kudhoofika kwa nguvu kazi ya taifa na kupungua kwa tija katika shughuli za uzalishaji mali, hususan miongoni mwa vijana ambao ndio nguvu kazi muhimu ya taifa.
“Dawa za kulevya si tatizo la mtu mmoja mmoja bali ni changamoto ya taifa zima. Athari zake zinaigusa jamii kwa ujumla na kuathiri maendeleo ya nchi katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.Amebainisha kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo kupitia operesheni za ukamataji, uchunguzi wa makosa ya dawa za kulevya, utoaji wa tiba kwa waathirika pamoja na kampeni za elimu kwa umma.
Kwa mujibu wa Lyimo, uchunguzi unaofanywa na mamlaka hiyo umebaini kuwa wahalifu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya wamekuwa wakibuni mbinu mpya za kuzisafirisha, ikiwemo kuzificha katika mizigo na vifurushi vinavyoonekana kuwa vya kawaida.
Amesema,baadhi ya wananchi wamejikuta wakikabiliwa na mkono wa sheria baada ya kukubali kubeba mizigo wasiyoifahamu kwa niaba ya watu wengine, bila kujua kuwa ndani yake kulikuwa na dawa za kulevya.
“Filamu hii imeandaliwa kuonesha uhalisia wa namna mtu anavyoweza kuingia kwenye mtego wa kuwa sehemu ya mtandao wa wahalifu kwa kubeba kifurushi au mzigo usiofahamu. Tunataka wananchi watambue kuwa mzigo unaoonekana wa kawaida unaweza kubeba dawa za kulevya na kubadilisha maisha yao kwa namna hasi,”amesema.Ameongeza kuwa,filamu hiyo itaanza kuoneshwa katika mabasi yanayofanya safari za mikoani kote nchini kwa ushirikiano wa DCEA, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Bodi ya Filamu Tanzania.
Hananja:Waraibu wasitengwe
Akizungumza katika hafla hiyo, Mchungaji Richard Hananja amesisitiza umuhimu wa jamii kutowatenga waraibu wa dawa za kulevya, akisema bado wana nafasi ya kurejea katika maisha ya kawaida na kulitumikia taifa.
Amesema,viongozi wa dini, wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kushiriki katika kuwaokoa waathirika wa dawa za kulevya kwa kuwaelekeza katika vituo vya tiba na huduma za kurejesha matumaini.
“Hawa ni watoto wetu.Tukiwatelekeza hatutakuwa tumetatua tatizo.Tanzania isiyo na dawa za kulevya inawezekana ikiwa wazazi, viongozi wa dini, Serikali na jamii tutashirikiana,”amesema Hananja.
LATRA yaunga mkono kampeni
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa LATRA, Halima Lutabi amesema,filamu hiyo ni ubunifu muhimu unaotumia nguvu ya sanaa kuelimisha jamii na kuchochea mabadiliko ya kitabia.

Amesema,sekta ya usafiri ni moja ya maeneo ambayo wahalifu wamekuwa wakiyatumia kusafirisha dawa za kulevya, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa abiria na kuharibu taswira ya sekta ya usafirishaji nchini.
“LATRA itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola na wadau wa usafirishaji kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazozuia matumizi ya vyombo vya usafiri katika shughuli haramu zinasimamiwa kikamilifu,”amesema.
TABOA yapongeza jitihada
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Abdallah Kiongozi amesema,filamu hiyo imekuja wakati muafaka kutokana na athari kubwa za dawa za kulevya kwa afya,uchumi na usalama wa taifa.
Ameahidi kuwa,chama hicho kitaendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kwa wanachama wake na kuhakikisha mifumo ya usafiri haitumiki kwa shughuli za usafirishaji wa dawa za kulevya.
“Tunapokea filamu hii kwa mikono miwili na tuko tayari kuisambaza kwa wanachama wetu ili kuongeza uelewa kuhusu hatari za dawa za kulevya,”amesema.
Filamu ni chombo cha mabadiliko
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga amesema,filamu imeendelea kuthibitisha kuwa nyenzo yenye nguvu katika kuelimisha na kuleta mabadiliko chanya ya kitabia katika jamii.
Amesema,taasisi za umma na binafsi zinapaswa kutumia zaidi sanaa na filamu kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa kuwa zina uwezo mkubwa wa kuhamasisha mabadiliko na kujenga maadili mema.
“Filamu hii itasaidia kuonesha madhara ya dawa za kulevya na kuwafanya wananchi kutambua hatari zilizopo katika kubeba mizigo au vifurushi wasivyovifahamu,”amesema.
Kwa ujumla, uzinduzi wa filamu ya “Kifurushi” umeonekana kuwa hatua mpya katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini, huku wadau wakisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi, sekta ya usafiri na taasisi za Serikali ni muhimu katika kuzuia usafirishaji wa dawa hizo na kulinda usalama wa jamii.
Ujumbe mkuu uliotolewa kwa wananchi ni kwamba wasikubali kubeba mzigo, kifurushi au bidhaa yoyote wasiyoifahamu, kwani kufanya hivyo kunaweza kuwahusisha na makosa makubwa ya jinai na kuathiri maisha yao pamoja na familia zao.Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni “Usafiri Salama Bila Dawa za Kulevya.”
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Filamu ya Kifurushi
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)






