Dkt.Natu Mwamba akutana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kujadili miradi ya kipaumbele ya IDA-21

DODOMA-Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe.Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Firas Raad ambapo wamejadili kuhusu miradi ya kipaumbele ya Serikali itakayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mzunguko wa 21 (IDA-21), kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa agenda ya maendeleo ya Taifa.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma, pande zote mbili zimejadili hatua za mwisho za kuidhinisha orodha ya miradi itakayojumuishwa katika mpango wa ufadhili wa IDA-21, huku Benki ya Dunia ikieleza kuridhishwa na ushirikiano unaoendelea kati yake na Serikali ya Tanzania katika kuandaa na kutekeleza miradi yenye matokeo chanya kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Bw. Firas Raad amesisitiza dhamira ya Benki ya Dunia kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopewa kipaumbele, akibainisha kuwa sekta ya nishati ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayopewa uzito mkubwa katika mzunguko huo wa ufadhili.

Ameeleza kufurahishwa na kujumuishwa kwa miradi mbalimbali ya nishati katika orodha ya miradi ya kipaumbele, jambo linaloendana na vipaumbele vya Benki ya Dunia vya kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za kijamii.

Aidha, Bw. Raad ametaja pia umuhimu wa miradi mingine ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Bonde la Mto Msimbazi, ambao umeendelea kupewa kipaumbele kutokana na mchango wake katika kuboresha mazingira, miundombinu na ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi katika Jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba ameeleza kuwa,Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Benki ya Dunia ili kuhakikisha miradi yote itakayopitishwa chini ya IDA-21 inatekelezwa kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia vipaumbele vya Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha ushirikiano na taasisi za maendeleo za kimataifa katika kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kukuza uchumi, kuongeza ajira, kuimarisha huduma za jamii na kuboresha maisha ya wananchi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, na Bw Robert Mtengule, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bi. Tiba Kisonga, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje - Zanzibar, Bw. Yussuf Ibrahim Yussuf, Meneja wa Uendeshaji wa Benki ya Dunia, Bi. Milena Stefanova na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here