MOROGORO-Viongozi mbalimbali wa Serikali, Jeshi la Polisi na viongozi wa dini wameungana me katika msiba wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard George Abwao, aliyekuwa akiagwa nyumbani kwake Mji Mwema, Nanenane mkoani Morogoro.
Miongoni mwa waliohudhuria ni Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda, Mhe. Denis Lazaro, pamoja na Makamanda wa Polisi kutoka mikoa ya Kinondoni, Mbeya, Iringa, Morogoro, Tanga na Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesoma wasifu wa marehemu na kuwashukuru viongozi, askari na wananchi waliojitokeza kumuaga marehemu, akisisitiza mshikamano uliooneshwa katika kipindi cha maombolezo.
Kwa niaba ya Serikali, Mhe. Denis Lazaro ametoa salamu za pole kutoka kwa Waziri Mkuu, Mhe. Mwigulu Nchemba, na kueleza kuwa marehemu alikuwa rafiki yake wa karibu tangu waliposoma pamoja katika Shule ya Sekondari Kigurunyembe.
Aidha, RPC Kinondoni, SACP Mtatiro, ambaye alikuwa mkuu wa msafara wa msiba na mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillius Wambura, ametoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.
Kwa niaba ya familia, kaka wa marehemu ameshukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano walioutoa tangu kipindi cha ugonjwa hadi maandalizi ya msiba. Mwili wa marehemu utapelekwa Tabora kabla ya kusafirishwa kwenda Mkoa wa Mara kwa ajili ya mazishi.




