Elimu ya fedha ni msingi wa ujumuishi wa kifedha-Naibu Gavana BoT

DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anayesimamia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha elimu ya fedha nchini ili kuwawezesha wananchi kutumia kwa ufanisi huduma mbalimbali za kifedha na hivyo kuongeza kiwango cha ujumuishi wa kifedha.
Akifungua Jukwaa la Elimu ya Fedha lililofanyika tarehe 29 Juni 2026 katika ofisi za BoT jijini Dar es salaam, Naibu Gavana alisema jukwaa hilo linatoa fursa muhimu ya kutathmini hatua zilizofikiwa katika kuifanya elimu ya fedha kuwa sehemu ya utaratibu endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Alieleza kuwa matokeo ya utafiti wa FinScope 2023 yanaonesha kuwa kiwango cha ujumuishi wa kifedha nchini kimefikia asilimia 76, mafanikio yaliyotokana kwa kiasi kikubwa na ukuaji wa huduma za fedha kwa simu.
Utafiti pia ulionesha kuwa uelewa wa fursa mbalimbali za huduma za kifedha na uwekezaji ulikuwa chini.

“Hata hivyo, juhudi zinazoendelea za kutoa elimu ya fedha ikiambatana na uhamasishaji wa fursa zilizopo zinaleta matunda, ambapo uelewa unakua kwa kasi kubwa,”ameeleza Naibu Gavana huyo.

Alisisitiza kuwa,utekelezaji wa programu ya Wakufunzi wa Elimu ya Fedha umeendelea kuleta mafanikio makubwa, ambapo hadi sasa jumla ya wakufunzi 1,736 wameidhinishwa kutoa elimu hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mafanikio hayo yametokana na ushirikiano madhubuti kati ya BoT na taasisi 14 za elimu zinazotekeleza programu ya mafunzo ya Wakufunzi wa Elimu ya Fedha, nazipongeza kwa mchango wao katika kuwajengea uwezo wataalamu watakaosaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya fedha.”
Aidha, alisema jitihada hizo zinaendana na Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21–2029/30 ulioandaliwa na Wizara ya Fedha, ambao unaweka msisitizo katika kuimarisha elimu na uelewa wa masuala ya fedha nchini.

Aliongeza kuwa kupitia Baraza la Taifa la Ujumuishi wa Huduma za Kifedha, wadau mbalimbali wameendelea kushirikiana kutekeleza Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha (NFIF III), ambapo elimu ya fedha imepewa nafasi ya kimkakati katika kuongeza matumizi ya huduma rasmi za kifedha.
Jukwaa hilo lenye kauli mbiu ‘Elimu ya fedha kwa maendeleo Yetu Sote’ limewakutanisha wadau kutoka sekta ya fedha, taasisi za elimu, Serikali na washirika mbalimbali kwa lengo la kutathmini mafanikio yaliyopatikana, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya fedha nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here