Wataalam wa Dunia wakusanyika Arusha kujadili utabiri wa hali ya hewa

ARUSHA-Tanzania imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa mwenyeji wa Warsha ya Nne ya Kimataifa ya masuala ya Utabiri wa Hali ya Hewa kwa Uendeshaji (The Fourth WMO International Workshop on Operational Climate Prediction-OCP4) iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) inayofanyika jijini Arusha kuanzia Juni 29 hadi Julai 03, 2026.
Akifungua warsha hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa aliishukuru WMO kwa kuileta warsha hiyo nchini na kubainisha kuwa hayo ni matokeo ya kuimarika na kuthamini masuala ya utabiri wa hali ya hewa nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Alisema warsha hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa nchi kutabiri hali ya hewa na tabianchi kwa usahihi zaidi ili tahadhari za mapema zinazookoa maisha, kulinda mali za watu na kusaidia kutoa maamuzi sahihi katika sekta muhimu kama vile kilimo, usafirishaji na maji ziweze kuchukuliwa.
Ameongeza kuwa warsha hiyo inakutanisha wataalamu wa fani tofauti kutoka nchi zaidi ya 20 duniani kubadilishana uzoefu, kujadili matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuboresha huduma za hali ya hewa zinazochangia maendeleo endelevu.

Prof. Mbarawa ametoa wito kwa washiriki wa warsha hiyo kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya utabiri na tahadhari ya mapema itakayokabiliana na athari za kuongezeka kwa matukio ya mafuriko, ukame, matetemeko na mawimbi ya joto yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi nchi duniani.

Waziri Mbarawa alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa kama vile akili unde ili kutoa utabiri wa haraka, sahihi na utakaoamimika.
Amehitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa Serikali imeimarisha huduma za hali ya hewa kwa kuwekeza katika miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na rada za kisasa, Kituo cha Kitaifa cha Hali ya Hewa, Kituo cha Uhakiki wa Hali ya Hewa na mifumo ya tahadhari ya mapema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here