HARARE-Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, amepokea taarifa ya maandalizi (briefing) kuhusu ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaotarajiwa kuanza tarehe 29 Juni, 2026 jijini Harare nchini Zimbabwe.
Wasilisho hilo liliwasilishwa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. James Msina, ambaye alimweleza Katibu Mkuu kuhusu ajenda kuu za mkutano, msimamo wa Tanzania katika maeneo mbalimbali ya majadiliano pamoja na masuala ya kimkakati yatakayojadiliwa na viongozi na wataalamu kutoka nchi wanachama wa SADC.Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha ujumbe wa Tanzania unashiriki kikamilifu katika mkutano huo, kwa kuwasilisha hoja zenye maslahi kwa Taifa na kuchangia mijadala itakayolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuongeza uwekezaji, biashara na ukuaji wa uchumi wa nchi wanachama.
Akizungumza baada ya kupokea wasilisho hilo, Dkt. Mwamba alisisitiza umuhimu wa maandalizi ya kina na uratibu mzuri ili kuhakikisha Tanzania inawakilishwa kwa ufanisi na kutoa mchango wenye tija katika majadiliano ya mkutano huo.
Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unatarajiwa kuanza kesho mjini Harare, ukiwakutanisha Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wataalamu wa Sekta za fedha, uwekezaji na afya kutoka nchi wanachama kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya ukanda wa Kusini mwa Afrika.


