DODOMA-Kufuatia mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamewezesha upatikanaji wa wawekezaji wa kujenga kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa bidhaa za chuma katika eneo la Nala jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa leo Juni 15,2026 na Waziri wa Madini,Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji wa Kampuni ya A1 Iron & Steel Tanzania Ltd ofisini kwake jijini Dodoma.
"Moja ya kipaumbele cha Serikali kwenye sekta ya madini ni uongezaji thamani wa madini. Hili ni eneo la kimkakati na tumelipa uzito mkubwa kuhakikisha tunafikia adhma ya kuondokana na kusafirisha nje madini ghafi.
"Uwekezaji huu utaogharimu takribani bilioni 600 unataraji kutumia chuma ghafi kama malighafi kuu ya kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo mabati, waya wa kufungia nondo, wavu wa nondo, misumari na nyinginezo," amesisitiza Mhe.Mavunde.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde amepongeza uwekezaji wa kiwanda hicho na kusisitiza kuwa unaendana na malengo ya dira ya nchi yetu wa kujitosheleza katika uzalishaji wa chuma na bidhaa zake utakaopelekea mageuzi katika uongezaji thamani ndani ya nchi na kupunguza gharama kwa watumiaji wa ndani.
Awali, akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya AI Iron & Steel Tanzania Ltd,Bw. Himanshu Tiwari ameeleza kuwa,kiwanda wanachokwenda kujenga kitakuwa cha mfano na aina yake kinachotumia teknolojia ya mlipuko wa tanuru (Blast furnace) inayowezesha na kurahisisha uzalishaji kuanzia hatua ya malighafi mpaka utaengenezaji wa bidhaa za mwisho.
Ujenzi huo unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15 kuanzia mwezi Julai, 2026 na unatarajiwa kuzalisha takribani ajira 1,500 na kupunguza utegemezi wa bidhaa za chuma kutoka nje ya nchi utakaosaidia kuongeza uwezo wa viwanda vyetu vya ndani na kuuza bidhaa za chuma nje ya nchi.



