NA DIRAMAKINI
TIMU ya Taifa ya Brazil imeanza kampeni yake ya Kombe la Dunia la FIFA 2026 kwa matokeo yasiyoridhisha baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Morocco katika mchezo wa Kundi C uliochezwa kwenye Uwanja wa MetLife mjini New Jersey, Marekani.
Picha na GM.
Brazil, mabingwa wa dunia mara tano, walijikuta wakipambana kusaka matokeo mbele ya Morocco maarufu kama Simba wa Atlas, ambao walionesha kiwango cha juu na nidhamu kubwa ya mchezo tangu dakika za mwanzo.
Morocco ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kiungo mshambuliaji Ismael Saibari katika dakika ya 21, akimalizia vyema shambulizi lililowashtua mabeki wa Brazil na kuiweka timu yake mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo liliwapa morali kubwa Wamorocco ambao waliendelea kucheza kwa kujiamini huku wakidhibiti sehemu kubwa ya eneo la kiungo na kuzuia mashambulizi mengi ya wapinzani wao.
Hata hivyo, Brazil waliongeza kasi ya mchezo kadri dakika zilivyosonga na kufanikiwa kusawazisha kupitia nyota wao Vinicius Junior katika dakika ya 32.
Mshambuliaji huyo alitumia vyema nafasi aliyoipata na kupeleka mpira wavuni, akiwarejeshea matumaini mashabiki wa mabingwa hao.
Aidha,baada ya mabao hayo mawili katika kipindi cha kwanza, timu zote zilirejea uwanjani kwa kipindi cha pili zikiwa na dhamira ya kusaka ushindi.
Brazil walionekana kutawala umiliki wa mpira kwa vipindi kadhaa, lakini walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa safu ya ulinzi ya Morocco iliyokuwa imara na yenye mpangilio mzuri.
Morocco nao waliendelea kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza yaliyowalazimu mabeki wa Brazil kufanya kazi ya ziada kuzuia hatari langoni mwao.
Pamoja na juhudi za pande zote mbili, hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao la ushindi hadi mwamuzi alipomaliza dakika 90 za mchezo.
Matokeo hayo yanaifanya Morocco kuendelea kuonesha kuwa ni moja ya timu zinazoweza kutoa ushindani mkubwa katika michuano hiyo, huku Brazil wakilazimika kusubiri mechi zijazo ili kuimarisha nafasi zao katika mbio za kutinga hatua ya mtoano.
Sare hiyo pia inaashiria ushindani mkali unaotarajiwa katika Kundi C, ambapo kila pointi inaweza kuwa muhimu katika kuamua timu zitakazofuzu hatua inayofuata ya mashindano.
