DAR-Serikali imeonya taasisi za umma zinazofanya vibaya kujitathmini na kuchukua hatua za haraka za kuboresha utendaji wao, ikisisitiza kuwa haitavumilia taasisi zitakazoendelea kuonesha utendaji duni kwa muda mrefu.
Onyo hilo lilitolewa na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, jijini Dar es Salaam Ijumaa, Juni 26, 2026, wakati wa mahojiano maalumu kuelekea Siku ya Gawio itakayofanyika Jumanne, Juni 30, 2026, katika Ikulu ya Dar es Salaam.
Bw. Mchechu alisema taasisi zote zinazostahili kuwasilisha gawio na michango mingine Serikalini zinapaswa kutekeleza wajibu huo kwa wakati, akisisitiza kuwa kushindwa kufanya hivyo ni kuinyima Serikali na wananchi mapato stahiki.
“Mashirika si mali ya bodi za wakurugenzi wala menejimenti, ni mali ya umma zinazosimamiwa na Serikali. Kwa muktadha huo, kurejesha kilicho haki ya wananchi si fadhila, bali ni wajibu,” alionya.
Alisisitiza kuwa viongozi wa taasisi za umma wanapaswa kuhakikisha malengo ya faida wanayopewa yanafikiwa ili kuongeza mchango wa taasisi hizo kwa uchumi wa taifa.
“Lazima taasisi zetu ziyaishi malengo ya faida ambayo huwa tunazipa. Mtu (kiongozi wa taasisi) ambaye ataendelea kushindwa kuleta gawio kwa kipindi kirefu, huyo hatufai,” alionya Bw. Mchechu.
Aidha, alisema gawio na michango mingine inapaswa kutokana na faida au ziada halisi ya taasisi, badala ya kukopa fedha, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kunatoa taswira isiyo sahihi kuhusu utendaji wa taasisi.
“Ukikopa ili utoe gawio au mchango mwingine kwa Serikali, unakuwa unamdanganya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na hata nafsi yako mwenyewe,” alisema.
Alipoulizwa iwapo taasisi zitakazoshindwa kufanya vizuri katika utoaji wa gawio mwaka huu zinaweza kufutwa, Bw. Mchechu alisema kufutwa au kuunganishwa kwa taasisi za umma ni mchakato endelevu unaofuata taratibu zilizowekwa, na si uamuzi unaotokana na matokeo ya Siku ya Gawio pekee.
“Hatufuti taasisi kwa sababu ya matokeo ya siku ya gawio. Tunazipa kwanza muda wa kufanya maboresho, na zisipoonyesha mabadiliko ndipo tunachukua hatua stahiki,” alifafanua Bw. Mchechu.
Katika mwaka wa fedha 2024/25, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) ilikusanya Sh1.028 trilioni kama gawio na michango mingine kutoka kwa taasisi za umma pamoja na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache, kiwango kilichoweka rekodi mpya tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo mwaka 1959.
Pamoja na mafanikio hayo, Bw. Mchechu alisema Serikali inaamini bado kuna fursa kubwa ya kuongeza makusanyo kwa kuimarisha utendaji wa taasisi za umma na usimamizi wa uwekezaji wa Serikali.
Akizungumzia matarajio ya siku zijazo, alisema OTR inaamini kuwa maboresho yanayoendelea katika ufanisi wa kiutendaji na kifedha wa taasisi za umma yataonekana katika matokeo ya mwaka huu wa fedha, huku mafanikio zaidi yakitarajiwa katika miaka ijayo.
“Tunategemea tutaanza na nguvu mpya, mwaka huu tutavunja rekodi ya mwaka jana na mwakani tutavunja rekodi ya mwaka huu,” alisema Bw. Mchechu.
Kauli za Bw. Mchechu zinaendana na msimamo wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, ambaye hivi karibuni alionya taasisi na mashirika ya umma yanayoendelea kuonesha utendaji usioridhisha kuwa yako hatarini kufutwa au kuunganishwa endapo hayataboresha utendaji wake.
Prof. Mkumbo alisema haiingii akilini kuona baadhi ya mashirika ya umma yakishindwa kutoa gawio stahiki licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.
Alisema Serikali itazipa taasisi husika muda wa kujirekebisha kabla ya kuchukua maamuzi ya kuziunganisha au kuzifuta pale itakapobidi.
“Ni afadhali kuwa na mashirika machache ya biashara, lakini yanayotoa gawio stahiki kwa Serikali,” alisisitiza Prof. Mkumbo.
Kwa mujibu wa OTR, Serikali inamiliki hisa katika taasisi na kampuni 308, ambapo 91 zinafanya shughuli za kibiashara huku 217 zikitoa huduma za umma.
Prof. Mkumbo alisema Serikali inataka kuona wananchi wakinufaika zaidi na uwekezaji wa Sh92.3 trilioni uliofanywa katika mashirika na taasisi za umma.
Ili kufanikisha azma hiyo, OTR imesema inaendelea kuimarisha usimamizi wa utendaji wa taasisi za umma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na usimamizi wa uwekezaji.
Bi. Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mashirika ya Kibiashara wa OTR, alisema ofisi hiyo imejipanga kuendelea kuimarisha utendaji wa taasisi za umma kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na usimamizi wa uwekezaji.
“Ni imani yetu kuwa usimamizi bora wa utendaji wa taasisi za umma ni msingi wa kuleta mageuzi endelevu katika uendeshaji wa taasisi na mashirika ya umma,” alisema Bi. Mauki.
Alisema usimamizi huo unatarajiwa kuchochea uzalishaji, kukuza uchumi na kuongeza mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, hatua itakayoimarisha uwezo wa serikali kutekeleza majukumu yake ya maendeleo na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, Bw. David Shambwe, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kibiashara wa OTR, alisema pamoja na mashirika hayo kutokuwa na lengo la kuzalisha faida, yanapaswa kuonyesha ufanisi katika utoaji wa huduma na matumizi ya rasilimali za umma.
Alisema OTR inaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya utendaji ili kuhakikisha mashirika hayo yanatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, uwajibikaji na kwa kuzingatia thamani ya fedha katika matumizi ya rasilimali za Serikali.
“Lengo letu ni kuona mashirika yasiyo ya kibiashara yanatoa huduma bora, zenye tija na zinazokidhi matarajio ya wananchi. Ufanisi wa taasisi hizi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa,” alisema Bw. Shambwe.
Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, akizungumza na Mwandishi wa Habari wa Azam TV, Kissa Daniel, wakati wa mahojiano maalum yaliyofanyika Ijumaa iliyopita katika makao makuu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, jijini Dar es Salaam.
Tags
Gawio Day
Gawio Day 2026
Gawio la Serikali
Habari
Nehemiah Kyando Mchechu
Ofisi ya Msajili wa Hazina



