ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa usimamizi wa ardhi kwa kuanzisha mfumo wa kidijitali wa usajili na matumizi ya ardhi, hatua itakayopunguza migogoro ya ardhi na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 28 Juni 2026, katika kilele cha Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Ardhi na Makaazi, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema Serikali imeamua kuanzisha Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi na Makaazi kutokana na umuhimu mkubwa wa sekta hizo katika maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi, hususan kwa Zanzibar ambayo ni nchi ya visiwa inayokabiliwa na changamoto ya ufinyu wa ardhi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali pia inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya nyumba za kisasa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya makaazi.
Ameeleza kuwa,nyumba 548 zinajengwa katika eneo la Kisakasaka B, nyumba 1,095 Kikwajuni, nyumba 1,095 Chumbuni na nyumba 22 katika eneo la Mombasa kwa Awamu ya Pili. Miradi mingine ni pamoja na Jengo la Biashara la Maisara na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo mengine ya Unguja na Pemba.
Amesema kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ni kubwa na nyumba hizo zinatarajiwa kufunguliwa wakati wa Sherehe za Mapinduzi mwaka 2027.
Aidha, Serikali inaandaa utaratibu utakaowawezesha wafanyakazi wa Serikali kumiliki nyumba kupitia mfumo wa mikopo.Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa upangaji bora wa matumizi ya ardhi ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya Zanzibar na ustawi wa wananchi.














