NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kushuka kwa bei kikomo za mafuta ya petroli nchini kuanzia Julai 1, 2026, kufuatia kupungua kwa bei za mafuta katika soko la dunia baada ya kupungua kwa mvutano wa kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Taarifa hiyo, imeeleza kuwa,makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati, pamoja na kuruhusu meli za mafuta kupita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, yamechangia kuanza kushuka kwa bei za mafuta katika soko la kimataifa.
Aidha, kampuni zinazochakata mafuta ghafi zimeendelea kuongeza ununuzi wa mafuta kutoka maeneo yasiyoathiriwa na migogoro ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa bidhaa hizo duniani.
Hata hivyo, EWURA imebainisha kuwa wastani wa bei katika soko la dunia bado haujafikia kiwango kilichokuwepo kabla ya kuanza kwa mgogoro huo mwishoni mwa Februari mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, bei za mafuta nchini zitashuka kwa Shilingi 96 kwa lita ya petroli, Shilingi 151 kwa lita ya dizeli na Shilingi 242 kwa lita ya mafuta ya taa.
Kwa mujibu wa bei kikomo mpya zitakazoanza kutumika saa 6:01 usiku wa Julai 1, 2026, katika Mkoa wa Dar es Salaam petroli itauzwa kwa Shilingi 3,990 kwa lita, dizeli Shilingi 4,182 na mafuta ya taa Shilingi 4,443 kwa lita.
Katika Mkoa wa Tanga, petroli itauzwa kwa Shilingi 4,051, dizeli Shilingi 4,243 na mafuta ya taa Shilingi 4,504 kwa lita, huku Mkoa wa Mtwara ukiwa na bei ya Shilingi 4,083 kwa petroli, Shilingi 4,275 kwa dizeli na Shilingi 4,536 kwa mafuta ya taa kwa lita.
EWURA imewataka wafanyabiashara wote wa mafuta kuzingatia bei kikomo zilizotangazwa na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka maelekezo hayo.
Mamlaka hiyo imekumbusha kuwa wananchi wanaweza kupata taarifa za bei kikomo za mafuta katika maeneo yao kwa kupiga namba 15200# kupitia mitandao yote ya simu nchini bila malipo.
Aidha, imeeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, bei za mafuta zinaendelea kuongozwa na ushindani wa soko, huku EWURA ikiendelea kuweka bei kikomo ili kulinda maslahi ya watumiaji na kuhakikisha ushindani wa haki katika biashara ya mafuta.
EWURA pia imevitaka vituo vyote vya mafuta kuweka mabango yanayoonesha bei za bidhaa zao sehemu zinazoonekana wazi kwa wateja, pamoja na kutoa stakabadhi za mauzo kupitia mashine za Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) kwa kila mnunuzi, hatua ambayo itarahisisha uthibitishaji wa bei, ubora wa mafuta na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Mamlaka hiyo imewahimiza wananchi kuchagua kununua mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu ndani ya viwango vilivyowekwa, ili kuimarisha ushindani na kuongeza uwazi katika soko la mafuta nchini.






