DAR-Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) leo tarehe 02 Julai, 2026 imefanya ziara ya kimkakati katika banda la Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana na kutoa mafunzo ya urasimishaji biashara kwa vikundi vya vijana vinavyoshiriki Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Katika ziara hiyo, Afisa Usajili wa BRELA, Bw. Benedickson Willson kutoka kurugenzi ya Miliki Ubunifu alitoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA katika kuwezesha wafanyabiashara, hususani kwenye usajili wa Alama za Biashara na Huduma.
Akizungumza baada ya kutoa elimu hiyo, Bw. Willson alisema mafunzo ambayo wamepata vijana hao yanalenga kuwasaidia wafanyabiashara hasa wabunifu wachanga kushindana kikamilifu katika soko la ndani na kimataifa
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa wafanyabiashara hasa vijana kama hawa kwani yanawapa uelewa wa kina kuhusu hatua za kusajili majina ya biashara, kampuni pamoja na kulinda nembo ambazo zinatambulisha bidhaa zao kwenye soko,”amesema Bw. Willson.
Aidha, Bw.Willson alibainisha kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Viwanda na Biashara kuzitaka taasisi zilizo chini ya Wizara kuwatembelea wafanyabiashara wanaoshiriki maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba na kuwasaidia kwa kuwapa huduma wezeshi.
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo, baadhi ya vijana wameshukuru BRELA kwa kuwpatia elimu hiyo huku wakibainisha kuwa itawasaidia kuendesha shughuli zao kwa kufuata misingi na taratibu za kisheria ikiwemo kulinda nembo zao na majina yao biashara ili yasitumiwe na watu wengine bila idhini yao.
“Leo tumetembelewa na BRELA, tumejifunza vitu vingi kuhusu huduma wanazotoa, wametushauri vijana kusajili na kulinda bunifu zetu kisheria kabla hatujaziendeleza kwa kiwango kikubwa kwani itatusaidia kuepuka changamoto za kisheria na mfanano wa majina au nembo pindi tutakapotaka kusajili."
BRELA imekuwa ikiwatembelea wafanyabiasha mbalimbali kwenye maonesho kama Sabasaba na kuwapa huduma za papo kwa papo pamoja na elimu juu ya huduma za usijali zinazotolewa ambapo katika mafunzo ya leo, wawakilishi wa vikundi tisa vya vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini wamenufaika.
