Mtumishi wa Hospitali ya Ocean Road akamatwa na dawa za kulevya,DCEA yatoa onyo kwa watumishi wa umma

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemkamata mtumishi wa Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam,Goodluck Erasto Nyakaselula (35) kwa tuhuma za kusafirisha kilogramu 106.04 za dawa za kulevya aina ya bangi kutoka nchini Kenya kuingia Tanzania.
Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo amewaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa,mtuhumiwa huyo ambaye ni mtaalamu wa picha za kitabibu (Radiographer) na mkazi wa Mbezi Beach, Dar es Salaam, alikamatwa mkoani Arusha akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Premio lenye namba za usajili T 853 ECX.

Amesema,kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni sehemu ya mafanikio ya operesheni zilizofanywa na DCEA katika kipindi cha Mei na Juni,mwaka huu, ambapo jumla ya watuhumiwa 188 walikamatwa kwa tuhuma mbalimbali zinazohusiana na biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Pia,amesema katika operesheni hizo, mamlaka hiyo ilikamata tani 22.6 za dawa za kulevya, lita 30.5 za bidhaa zenye viambata vya dawa za kulevya na kilogramu 19.94 za dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Aidha, DCEA iliteketeza ekari 228.5 za mashamba ya bangi pamoja na tani 3.3 za bangi na mirungi, huku magari sita, bajaji mbili na pikipiki 33 zilizokuwa zikitumika katika shughuli za uhalifu huo zikikamatwa.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema,operesheni zilizofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) pia zilibaini kilogramu 19.94 za bidhaa zilizoingizwa nchini kama virutubisho vya lishe aina ya AFA CELL (Moringa Extract).
Amesema,uchunguzi wa maabara ulithibitisha kuwa bidhaa hizo zilikuwa na kiambata cha dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Prazepam, ambayo matumizi yake yasiyo sahihi yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya.

Katika operesheni nyingine,DCEA ilikamata gramu 972.05 za mirungi katika eneo la ukaguzi wa mizigo wa bandari ya boti zinazotoa huduma kati ya Dar es Salaam na Zanzibar. Mirungi hiyo ilikuwa ikisafirishwa na Kalsam Abdurahman Sebbi (43), raia wa Kenya mwenye makazi yake Mombasa.

Wilayani Kigamboni, mamlaka hiyo ilikamata gramu 162.48 za heroin na kumkamata mtuhumiwa Omary Miraji Mbonaeni.

Aidha, katika kituo cha mabasi wilayani Same mkoani Kilimanjaro, DCEA ilikamata kilogramu 240 za mirungi zilizokuwa zimefichwa ndani ya mabegi ya nguo, huku Irene Obedi Sule na Eliasi Obedi Sule wakitiwa mbaroni.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema,operesheni zilizofanyika katika mikoa mingine nchini zilisababisha kukamatwa kwa tani 19.5 za bangi, tani 2.6 za mirungi, kilogramu 40 za skanka na gramu 11.63 za heroin.

Ameongeza kuwa,tani 3.3 za bangi na mirungi pamoja na ekari 228.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika wilaya za Chamwino mkoani Dodoma, Kilwa mkoani Lindi pamoja na Sengerema na Geita.
Kamishna Jenerali Lyimo amewataka watumishi wa mashirika na taasisi za umma kuzingatia maadili ya utumishi na kujiepusha na biashara ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa sheria itachukua mkondo wake bila kujali hadhi ya mtu.

"Watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kulinda sheria na maadili ya nchi. Tunatoa onyo kwa wote wanaojihusisha au wanaofikiria kuingia katika biashara ya dawa za kulevya kuwa sheria ni msumeno; itamfikia yeyote atakayebainika kujihusisha na uhalifu huo,"amesema Kamishina Jenerali Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here