Serikali kuanza kutoa vibali vya ujenzi kwa wamiliki waliotayari kushiriki mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza jijini Dar es Salaam

DAR-Serikali imetangaza kuanza kutoa vibali vya ujenzi na kufanya majadiliano na wamiliki wa ardhi na nyumba ambao wapo tayari kushiriki kwenye Mpango wa Uendelezaji Upya eneo la Sinza, huku ikisisitiza kuwa mchakato uliopita umefutwa ili kutoa nafasi ya kuanza upya kwa misingi ya uwazi, ushirikishwaji na kujenga maridhiano.
Kauli hiyo ilitolewa Julai 1, 2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, alipokutana na wamiliki wa ardhi na nyumba wa Sinza kwa lengo la kuwafafanulia hatua za utekelezaji wa mpango huo na kusikiliza maoni yao.

Dkt. Akwilapo alisema Serikali imeamua kufungua ukurasa mpya baada ya kubaini kuwa mchakato uliopita uliacha malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi, hivyo vikao vyote vya awali vimefutwa na sasa mazungumzo yanaanza upya kwa ushirikiano na wananchi.
Alieleza kuwa ukuaji wa miji ni jambo lisiloepukika kutokana na ongezeko la watu na mahitaji ya makazi, hivyo Serikali ina wajibu wa kupanga matumizi ya ardhi kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Waziri huyo alisema Sinza ya sasa imebadilika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya nyuma, jambo ambalo linahitaji mpango mpya wa maendeleo utakaoendana na hadhi yake kama eneo muhimu la makazi na biashara ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

"Kama mwananchi anaona mpango huu haufai, hiyo ni haki yake, lakini ipo siku ataona umuhimu wake. Tusiporatibu maendeleo ya miji, tutakuwa na maeneo yasiyo na mpangilio na yenye miundombinu isiyokidhi mahitaji ya wananchi,"alisema.

Dkt. Akwilapo alibainisha kuwa uendelezaji upya wa maeneo ya makazi si jambo geni nchini, kwani maeneo kama Posta, Kariakoo, Upanga, Oysterbay na Masaki yamepitia hatua kama hizo na yameendelea kuwa na thamani kubwa zaidi kutokana na upangaji mzuri wa matumizi ya ardhi.
Waziri huyo aliwataka wananchi kuwa makini na watu wasio waaminifu wanaoweza kutumia mchakato huo kuwahadaa au kuwasambazia taarifa zisizo sahihi kwa manufaa binafsi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema mafanikio ya mpango huo yatategemea kiwango cha ushirikishwaji wa wananchi na kuzingatia maoni yao.

Alipendekeza muda wa ukusanyaji wa maoni uongezwe kwa miezi mitatu ili wananchi wengi zaidi wapate nafasi ya kuelewa mpango huo na kutoa maoni yao kabla ya hatua za utekelezaji kuanza.

"Wananchi wasikilizwe, maoni yao yazingatiwe na rasimu iboreshwe ili iakisi matakwa yao. Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haiwezi kupora haki za wananchi bali itafuata sheria, kanuni na taratibu zote zinazotambuliwa,"alisema Profesa Mkumbo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga aliwataka wamiliki wa ardhi na nyumba wa Sinza kuwa watulivu na kutochukua maamuzi ya haraka ya kuuza maeneo yao kutokana na taarifa zisizo rasmi.

Alisema thamani ya ardhi katika eneo la Sinza imeongezeka maradufu hivyo wananchi wanapaswa kutambua fursa iliyopo badala ya kufanya maamuzi yatakayowagharimu baadaye.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Wamiliki wa Ardhi na Nyumba wa Sinza, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Asibwene Lumuli, alisema ushirikiano kati ya Serikali na wananchi ndio utakaohakikisha mpango huo unatekelezwa kwa mafanikio na kwa manufaa ya pande zote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here