Dereva (fundi mkuu) ahukumiwa kwa wizi wa magurudumu ya Halmashauri ya Wilaya ya Chemba

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma kwa niaba ya Jamhuri, imeshinda Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 12183/2026 dhidi ya Salum Juma Iddi, Dereva (Fundi Mkuu) wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, baada ya Mahakama ya Wilaya ya Chemba kumtia hatiani kwa kosa la wizi wa magurudumu saba ambayo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
Ilielezwa mahakamani kuwa mshtakiwa, mnamo Oktoba 12, 2024, aliandaa nyaraka za uongo zikionesha kuwa gari lenye namba za usajili SM 2721 lilikuwa limefungwa magurudumu saba mapya kwa ajili ya shughuli za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ilhali akifahamu kuwa magurudumu hayo hayakuwa yamefungwa kwenye gari hilo.

Aidha, alipokea na kuchukua mali hiyo bila kuwa na haki ya kufanya hivyo, huku akijua kuwa ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.

Kesi hiyo ilisikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Chemba, Mheshimiwa Andrew Hayuma, huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Mawakili wa Serikali Dickson Misanjo na Happiness Mfungo kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma.

Katika hukumu iliyotolewa Juni 29, 2026, mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa moja la wizi unaofanywa na mtumishi wa umma, kinyume na Kifungu cha 270 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2023.

Baada ya kutiwa hatiani, mahakama ilimhukumu mshtakiwa kulipa faini ya shilingi 50,000 na kurejesha kiasi cha shilingi 2,500,000 kama fidia kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, ikiwa ni thamani ya mali iliyoibiwa.

Mshtakiwa ametekeleza amri ya mahakama kwa kulipa faini pamoja na kurejesha kiasi cha fedha alichoamuriwa kama fidia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here