TANGA-Mahakama ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga mbele ya Mhe. Stephano Mkoye Kushaba imemtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la wizi akiwa mtumishi wa umma kinyume na kifungu cha 258 (1)(2)(a), 265 na 270 vya kanuni za adhabu Sura 16 marejeo ya mwaka 2022 katika kesi ya jinai namba 7073/2026.
Baada ya kutiwa hatiani, mshtakiwa alipewa adhabu ya kifungo cha nje mwaka mmoja na kuamuliwa kurejesha kiasi cha shilingi 430,000 ikiwa ni sehemu ya fedha alizofanyia ubadhirifu.
Ilidaiwa kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti akiwa anatekeleza jukumu la kukusanya mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Handeni kwa kutumia mashine ya POS.
Ambapo wakati anatekeleza jukumu hilo alikusanya kiasi cha shilingi 2,616,950 na akazitumia kwa manufaa yake binafsi badala ya kuziwasilisha benki kwenye akaunti ya Halmashauri.
Hukumu ilitolewa na hakimu huyo mbele ya Reuben Ngassa, mwendelesha mashtaka wa TAKUKURU baada ya mshtakiwa kufanya makubaliano ya kukiri kosa katika ofisi ya mashtaka.
