NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA ya Wilaya ya Iringa imemtia hatiani dereva wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Pancras Mushara Prosper baada ya kupatikana na hatia ya kuomba rushwa ya Shilingi 600,000 ili kushawishi mwenendo wa shauri la ndoa na talaka lililokuwa likisikilizwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Iringa Mjini.

Hukumu hiyo imetolewa Julai 2,2026 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Benedict Nkomola katika Kesi ya Jinai Na. 23785/2026 kati ya Jamhuri dhidi ya Pancras Mushara Prosper.
Mahakama ilimkuta mshtakiwa na hatia ya kosa la kuomba rushwa, kinyume na Kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2022.
Baada ya kutiwa hatiani, mahakama ilimhukumu kulipa faini ya Shilingi 500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani. Mshtakiwa alilipa faini hiyo na hivyo kuepuka kifungo.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 12,2024 alipomuomba Wilbert Evaristo Simango kiasi cha Shilingi 600,000 kupitia simu, akidai fedha hizo zingemwezesha kumsaidia katika shauri la ndoa na talaka lililokuwa likiendelea katika Mahakama ya Mwanzo ya Iringa Mjini.
Ilielezwa kuwa, kitendo hicho kilihusiana na majukumu ya kikazi ya mshtakiwa, jambo lililokiuka sheria za kuzuia na kupambana na rushwa.
Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Salum Bhoki na Kassim Mussa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa.