Serikali yaridhishwa na maendeleo ya miradi ya nyumba za watumishi wa umma Kigoma

NA ANTONIA MBWAMBO

SERIKALI imeeleza kuridhishwa na Maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Watumishi wa Umma Awamu ya Pili katika Mkoa wa Kigoma kufuatia ukaguzi uliofanywa na timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Watumishi Housing Investiments.
Hayo yamesemwa Julai 2,2026 na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini Bw. Patrick Allute, wakati wakihitimisha ziara ya ukaguzi wa miradi ya makazi ya Watumishi wa Umma mkoani Kigoma ambapo timu ilikagua mradi ya nyumba za Watumishi katika Shule ya Sekondari Muhunga, Wilaya ya Kasulu, na Kituo cha Afya Muyama, Wilaya ya Buhigwe,Mkoa wa Kigoma.

Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara hiyo, Bw. Allute amepongeza wasimamizi wa mradi, Watumishi Housing na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa usimamizi unaowezesha miradi hiyo kutekelezwa kwa ufanisi.
Amesema, hatua iliyofikiwa inaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha mazingira ya kazi na ustawi wa Watumishi wa Umma.

Aidha, ameutaja mradi wa nyumba za Watumishi katika Kituo cha Afya Muyama kuwa miongoni mwa miradi iliyofanya vizuri zaidi kati ya miradi 15 iliyokaguliwa katika Mikoa mbalimbali ya Tanzania kutokana na kasi ya utekelezaji na ubora wa kazi inayoendelea kuonekana.

"Mradi wa nyumba za Watumishi katika Kituo cha Afya Muyama umeonesha kiwango cha juu cha utekelezaji. Kazi nyingi muhimu, ikiwemo mfumo wa umeme, zimekamilika na mradi umebakiza hatua chache kabla ya kukamilika na kuanza kutumika,"amesema Bw. Allute.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa Kituo cha Afya Muyama ameishukuru timu ya ukaguzi kwa ushauri na maelekezo yaliyotolewa, akisema yataendelea kufanyiwa kazi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa Watumishi wa Umma waliokusudiwa kunufaika nao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here