JWTZ latoa hakikisho kuhusu usalama wa nchi,lawaonya wanaochochea vurugu

NA DIRAMAKINI

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewahakikishia Watanzania kuwa, hali ya usalama na mipaka ya nchi ipo shwari, huku likiwataka wananchi kupuuza wito wowote unaohamasisha vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa na ustawi wa wananchi.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Sylvester Mangure ambaye amesema,hali ya utulivu iliyopo nchini imetokana na uzalendo wa wananchi pamoja na ushirikiano wao na vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda amani na mshikamano wa Taifa.

Amesema,mazingira hayo ya amani yamewawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku za uzalishaji na ujenzi wa Taifa bila hofu.

Hata hivyo, JWTZ limeeleza kuwa limebaini kuwepo kwa watu wanaoendesha kampeni za upotoshaji na uchochezi kwa lengo la kuwashawishi wananchi kushiriki katika vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani, huku wakilitumia vibaya jina la Jeshi kwa kudai kuwa litakuwa sehemu ya kulinda au kuunga mkono vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, taarifa hizo ni za upotoshaji na zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa washiriki na wananchi wengine, ikiwemo kuharibu mali, kuvuruga shughuli za kiuchumi na kuhatarisha usalama wa taifa.

JWTZ limewasihi wananchi kutoshiriki katika aina yoyote ya vurugu au matendo yanayoweza kuvuruga utulivu wa nchi, badala yake waendelee na shughuli zao za kila siku kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Aidha, jeshi hilo limesisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayehusika na vitendo vya uvunjifu wa amani, likieleza kuwa lina wajibu wa kikatiba wa kulinda nchi na wananchi wake.

Limefafanua kuwa,kwa mujibu wa Ibara ya 147(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, JWTZ limepewa jukumu la kulinda usalama wa nchi na wananchi, huku Kifungu cha 22 cha Sheria ya Ulinzi wa Taifa, Sura ya 192, kikiliruhusu kusaidia mamlaka za kiraia pale kunapotokea vurugu,ghasia au uvunjifu wa amani.

Katika taarifa hiyo, JWTZ pia limewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji, mitaa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu viashiria vyovyote vya uchochezi au vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi ili hatua za mapema ziweze kuchukuliwa.

Jeshi hilo limewahakikishia Watanzania kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda nchi, Katiba na mamlaka ya dola kwa weledi, utii, uaminifu na uzalendo mkubwa, huku likiendelea kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kudumisha amani, umoja na maendeleo ya Taifa. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here