NA DIRAMAKINI
MWINJILISTI wa Kimataifa, Dkt.Alphonce Temba amesema suluhisho la kudumu la msongamano wa magari hususan malori katika Jiji la Dar es Salaam, si kuendelea kuunda kamati za ushauri bali ni kutekeleza kikamilifu mipango ya Serikali ya kuhamishia shughuli za bandari kavu katika Kituo cha Kimkakati cha Kwala na maeneo mengine yaliyopangwa nje ya jiji.
Dkt.Temba alitoa kauli hiyo alipokuwa akichangia mada katika kipindi cha Kipima Joto cha runinga ya ITV kilichojadili suala la viongozi wa Serikali kuendelea kutoa matamko kuhusu foleni za Dar es Salaam bila kuona utekelezaji wa kudumu wa maamuzi hayo.Amesema,Tanzania inapaswa kutekeleza kwa vitendo mipango ya muda mrefu ya maendeleo ya miji badala ya kuendelea kujadili suluhisho ambalo tayari lilifanyiwa maamuzi miaka mingi iliyopita.
Kwa mujibu wake, tangu mwaka 2008 na 2009, wakati wa Serikali ya Waziri Mkuu mstaafu Peter Pinda, Bunge lilipitisha mpango wa kuanzisha mzani katika eneo la Vigwaza pamoja na kuendeleza Kwala kuwa kitovu cha bandari kavu, hatua iliyolenga kupunguza msongamano wa malori katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Amesema,mipango hiyo pia imo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, lakini bado haijatekelezwa kikamilifu kutokana na kile alichodai kuwa ni mgongano wa maslahi ya baadhi ya watu wanaonufaika na uwepo wa bandari kavu ndani ya jiji.
"Tunapaswa kunyoosha mambo.Hii nchi ni yetu sote. Haiwezekani tuendelee kuzungumza kila siku kuhusu foleni wakati suluhisho lipo wazi. Kwala ilipangwa kwa kazi hiyo muda mrefu," amesema.
AHOJI UUNDWAJI WA KAMATI
Dkt.Temba ameeleza kuwa,baadhi ya watu wanaopewa jukumu la kushauri namna ya kutatua changamoto ya foleni wanaweza kuwa na maslahi ya moja kwa moja katika biashara ya maghala na yadi za kuhifadhi makontena ndani ya Dar es Salaam, jambo ambalo linaweza kuathiri ushauri wanaoutoa.
Amesema,wamiliki wa yadi hizo hupata mapato makubwa kutokana na upangishaji wa maeneo ya kuhifadhi makontena, hivyo hawawezi kushawishi kuhamishwa kwa shughuli hizo kwenda Kwala au maeneo mengine yaliyopangwa.
"Ukimpa mtu mwenye yadi ya makontena jukumu la kushauri namna ya kuondoa malori mjini, unategemea atashauri nini? Atakuwa analinda biashara yake,"amesema.
ATOA MFANO WA AFRIKA KUSINI
Akizungumzia upangaji wa miji, Dkt.Temba amesema mataifa mengi duniani yamewekeza katika maendeleo ya miji satelaiti (Satellite Cities) ili kupunguza msongamano wa shughuli katikati ya miji mikubwa.
Ametolea mfano Afrika Kusini ambapo amesema safari kati ya Pretoria na Johannesburg yenye umbali wa takribani kilometa 58 huchukua chini ya saa moja kutokana na uwepo wa miundombinu bora ya usafiri wa reli na barabara.
Amesema,Tanzania inapaswa kuharakisha utekelezaji wa miji mipya kama Kwala, Vigwaza, Chalinze na Morogoro ili shughuli za biashara na usafirishaji zisirundikane ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
AKOSOA BANDARI KAVU NDANI YA JIJI
Aidha,ameeleza kuwa maeneo yaliyokuwa yakitumika kwa shughuli za kijamii sasa yamegeuzwa kuwa sehemu za kuhifadhi makontena na magari.
Ametaja eneo la Jangwani ambalo kwa miaka mingi lilikuwa likitumika kwa mikutano mikubwa ya kitaifa, kisiasa na kidini akisema sasa limejaa makontena.
Vilevile amelitaja eneo la Biafra ambalo kwa sasa linatumika kuhifadhi magari badala ya matumizi ya awali ya wananchi.
Kwa mtazamo wake, hali hiyo inaonesha kukosekana kwa utekelezaji wa mipango rasmi ya matumizi ya ardhi.
AHIMIZA KUTEKELEZWA KWA MPANGO WA KWALA
Dkt.Temba amesema,tayari Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 90 katika maendeleo ya Kwala, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuanzisha bandari kavu mpya ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Pia,amesema mataifa jirani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Sudan yanaonesha nia ya kutumia Kwala kama kitovu cha shughuli zao za usafirishaji wa mizigo, jambo litakaloifanya Tanzania kuwa kitovu kikubwa cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ameongeza kuwa,kuendelea kuruhusu malori kuingia katikati ya jiji kunachangia msongamano mkubwa wa magari,matumizi makubwa ya mafuta, ucheleweshaji wa shughuli za kiuchumi na hasara kubwa kwa taifa.
"Tunapoteza mabilioni ya fedha kila siku kutokana na foleni.Watu wanatumia muda mwingi barabarani badala ya kufanya shughuli za uzalishaji,"amesema.
DRC YAWEKEZA KWALA
Kwa mujibu wa taarifa rasmi za ushirikiano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nchi hiyo imetenga uwekezaji wa takribani dola za Marekani milioni 291.3 kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa bandari kavu ya Kwala kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.
Mradi huo unatarajiwa kujengwa katika eneo la Kwala lililopo takribani kilometa 60 kutoka Bandari ya Dar es Salaam, ambapo DRC imepewa eneo la hekta 45 kwa ajili ya shughuli zake za usafirishaji wa mizigo.
Bandari hiyo inatarajiwa kupunguza muda wa usafirishaji wa mizigo ya Congo kupitia Bandari ya Dar es Salaam kutoka wastani wa siku 15 hadi 16 na kufikia siku tano hadi sita, huku ikipunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ufanisi wa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaeleza kuwa,utekelezaji kamili wa mradi wa Kwala unaweza kuwa hatua muhimu katika kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya Tanzania kuwa kitovu kikuu cha biashara na usafirishaji wa mizigo katika eneo la Afrika Mashariki,Kusini na Kati.
Tags
Bandari Kavu Kwala
Bandari ya Kwala
Dr Alphonce Boniface Temba
Habari
Kongani ya Viwanda Kwala
Mwinjilisti Alphonce Temba