Mkalama yatoa mikopo ya shilingi milioni 500, yaongeza shule,vituo vya afya na uzalishaji katika kilimo ndani ya mwaka mmoja

NA DIRAMAKINI

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida imeendelea kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi katika mwaka wa fedha 2025/26, ikiwemo kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 500 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kuongeza miundombinu ya elimu na afya, pamoja na kuimarisha uzalishaji wa kilimo na mifugo.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama,Hajjat Asia Juma Messos ameyasema hayo leo Julai 2,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya mwaka mmoja ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2025/2026.

Amebainisha kuwa,mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali pamoja na usimamizi mzuri wa rasilimali za maendeleo.

Katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, Halmashauri ilitoa mikopo ya asilimia 10 yenye thamani ya Shilingi 500,598,000 kwa vikundi 52, ambapo vikundi 24 vya wanawake vilipokea Shilingi 208,011,000, vikundi 19 vya vijana Shilingi 259,787,000 na vikundi tisa vya watu wenye ulemavu Shilingi 32,800,000.

Sambamba na hilo,Hajjat Messos amesema, halmashauri ilianzisha huduma ya MAK (Mkalama Asilimia Kumi Kliniki), mfumo wa kliniki tembezi unaosogeza huduma za mikopo katika ngazi ya vijiji.

Kupitia mpango huo, wananchi zaidi ya 2,000 walifikiwa kupitia mikutano ya hadhara katika kata 17 na vijiji 70, huku mamilioni ya wananchi wakifikiwa kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya mikopo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, wanachama 289 kutoka vikundi mbalimbali walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara, hatua iliyochangia kuongeza ajira, kipato na shughuli za kiuchumi ndani ya wilaya.

Pia katika sekta ya biashara, amesema halmashauri ilifanya ukaguzi wa maduka 560 kwa lengo la kutoa elimu na kuboresha mazingira ya biashara, huku idadi ya wawekezaji ikiongezeka kutoka sita mwaka 2024/25 hadi tisa kufikia Juni 30,2026.

Vilevile,Sekta ya Elimu imeendelea kushuhudia mafanikio makubwa baada ya halmashauri kujenga shule mpya nne, zikiwemo shule mbili za sekondari za Kinyambuli na Kidarafa pamoja na shule mbili za msingi za Mlumba na Gracemesaki kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.3.

Aidha, madarasa 34, maabara tano na bweni moja vilijengwa kwa gharama ya Shilingi milioni 305, huku idadi ya shule za Kidato cha Tano na Sita ikiongezeka kutoka tatu hadi sita.

Kwa sasa halmashauri ina shule 99 za msingi na shule 22 za sekondari ambapo kwa upande wa matokeo ya kitaaluma, ufaulu wa Kidato cha Nne umeongezeka kutoka asilimia 97.89 mwaka 2024 hadi asilimia 97.91 mwaka 2025, huku shule zote za Kidato cha Tano na Sita zikidumisha ufaulu wa asilimia 100.

Pia, ufaulu wa Darasa la Saba umeongezeka kutoka asilimia 68 hadi asilimia 71.85.

Hajjat Messos anesema,Serikali pia ilitoa ruzuku ya elimu yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.69, pamoja na vitabu vya kiada 45,848 na vifaa vya TEHAMA 115, huku walimu wapya 65 wakiajiriwa ili kupunguza upungufu wa walimu.

Katika sekta ya afya,amesema halmashauri imejenga zahanati nne na inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya Iguguno pamoja na ukarabati wa miundombinu mbalimbali kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 719.

Upatikanaji wa dawa umeongezeka kutoka asilimia 92 hadi asilimia 93.8 baada ya kununuliwa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 850, huku mashine mpya 11 za uchunguzi na vifaa tiba vya Shilingi milioni 200 vikisambazwa katika vituo vya afya.

Huduma za matibabu bila malipo zimeendelea kutolewa kwa wazee wenye umri wa miaka 60 na zaidi pamoja na watoto chini ya miaka mitano. Katika mwaka uliopita, wazee 5,501 na watoto 15,664 walinufaika na huduma hizo, zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 104.

Katika sekta ya kilimo, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 116,948 hadi tani 354,438, huku uzalishaji wa mazao ya biashara ukiongezeka kutoka tani 44,796 hadi tani 50,471.

Mafanikio hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa maafisa ugani, matumizi ya mbegu bora na mbolea za ruzuku zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 9.4, pamoja na matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani uliobooresha soko la zao la dengu.

Sekta ya mifugo nayo imeendelea kuimarika baada ya mifugo zaidi ya 173,000 kupatiwa chanjo na matibabu, huku uzalishaji ukiongezeka kutoka asilimia 65 hadi asilimia 80.

Katika uhifadhi wa mazingira, Halmashauri ilisambaza majiko 4,370 ya nishati safi, yakiwemo majiko ya gesi na banifu, pamoja na kupanda miti zaidi ya 800,000 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Katika kuimarisha utumishi wa umma, amesema halmashauri iliajiri watumishi wapya 344 katika sekta mbalimbali, huku watumishi 216 wakipandishwa madaraja kwa kuzingatia sifa na utendaji wao.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, amesema halmashauri imepanga kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Ishenga kupitia mradi wa SEQUIP, ukamilishaji wa Hospitali ya Wilaya, vituo vya afya vya Ilunda na Gumanga, pamoja na ujenzi wa nyumba za wakuu wa idara na miundombinu mingine ya elimu na afya.

Halmashauri imesema itaendelea kuweka kipaumbele katika kuboresha huduma za elimu, afya, kilimo, mifugo na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, sambamba na kuhimiza watumishi kuongeza uwajibikaji na ubunifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here