NA DIRAMAKINI
MWINJILISTI wa Kimataifa, Dkt.Alphonce Temba amewataka Watanzania kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa utulivu na kutoingiwa na hofu kutokana na taarifa zinazosambaa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu uwezekano wa kufanyika maandamano, akisisitiza kuwa amani na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza leo Julai 6, 2026, Dkt.Temba amesema,ameamua kuzungumza na wananchi kwa mara ya pili kufuatia kuibuka tena kwa taarifa zinazohamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii.Amekumbusha kuwa,kabla ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru ya Desemba 9,2025 aliwahi kutoa wito kama huo na kufanya maombi ya kuliombea Taifa ili kuendelea kudumisha amani.
Amesema,ana imani kuwa Watanzania wataendelea kuzingatia amani na kufanya shughuli zao za maendeleo bila kuvurugwa na taarifa zinazoweza kuleta taharuki.
"Ninawaomba Watanzania waendelee na shughuli zao za kila siku.Tuendelee kulinda amani yetu na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa Taifa,"amesema.
Dkt.Temba amesema,taarifa za maandamano zinazosambazwa mara kwa mara kupitia mitandao ya kijamii zinaweza kusababisha taharuki isiyo ya lazima kwa wananchi na kuongeza mzigo kwa vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo hulazimika kuelekeza nguvu katika maandalizi ya kukabiliana na hali hiyo.
Amesema,Tanzania imeendelea kujijengea sifa ya kuwa miongoni mwa nchi zenye amani na utulivu barani Afrika, jambo ambalo limechangia kuvutia uwekezaji, kukuza uchumi na kuimarisha mshikamano wa wananchi.
Katika maelezo yake,Dkt.Temba ametoa mifano ya baadhi ya mataifa aliyowahi kutembelea akieleza kuwa nchi nyingi zimeendelea kuwa na utulivu kutokana na kuheshimu misingi ya sheria na amani, huku akisisitiza kuwa Tanzania inapaswa kuendelea kulinda sifa hiyo.
Mbali na hilo,amesema kwa mtazamo wake changamoto zinazojitokeza nchini hazipaswi kutazamwa kwa mtazamo wa kijamii na kisiasa pekee, bali pia zinahitaji kuombewa,akiamini kuwa viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kuhamasisha amani,maadili na mshikamano wa kitaifa.
Amesema,viongozi wa dini wana wajibu wa kuendelea kuwaombea viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla ili nchi iendelee kuwa na utulivu na mazingira bora ya maendeleo.
Dkt.Temba pia ametoa wito kwa wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa au zinazoweza kuchochea taharuki na migawanyiko katika jamii.
Aidha,amewataka viongozi wa dini, taasisi mbalimbali pamoja na wananchi kuendelea kushirikiana katika kulinda umoja wa Taifa, akisisitiza kuwa maendeleo ya Tanzania yanategemea uwepo wa amani, utulivu na mshikamano.
Kauli yake imekuja katika kipindi ambacho vyombo vya dola vimeendelea kutoa wito kwa wananchi kuzingatia sheria,kulinda amani na kuendelea na shughuli zao za kila siku huku vikisisitiza kuwa usalama wa nchi unaendelea kuwa imara.

