DAR-Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab A. Katimba (Mb) ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026).
Mhe.Katimba ametoa pongezi hizo Julai 1, 2026 baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililopo katika Ukumbi wa Karume ndani ya Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, vinakofanyika maonesho hayo.
Amesema,ushiriki wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maonesho hayo ni hatua muhimu ya kuwaletea wananchi huduma na elimu ya kisheria kwa ukaribu zaidi, jambo linalochangia kuongeza uelewa wa umma kuhusu haki zao na huduma zinazotolewa na Serikali.
Mhe. Katimba amewahimiza maafisa wa ofisi hiyo kuendelea kutumia maonesho hayo kama fursa ya kutoa elimu ya sheria na kuwahudumia wananchi kwa weledi, ili kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia Watanzania wengi zaidi.
Kwa upande wake, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake, huduma mbalimbali za kisheria pamoja na ushauri unaotolewa kwa Serikali kupitia banda lake katika maonesho hayo.
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yalianza Juni 28, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026, yakitoa jukwaa kwa taasisi za umma na sekta binafsi kuonesha huduma, bidhaa na ubunifu mbalimbali kwa wananchi.
Tags
Habari
Maonesho ya Sabasaba 2026
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Wizara ya Katiba na Sheria
