DAR-Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu,Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kusogeza huduma za ushauri wa kisheria kwa wananchi kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026).
Prof. Kabudi ametoa pongezi hizo Julai 4, 2026, baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililopo katika Ukumbi wa Karume ndani ya Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, vinakoendelea maonesho hayo.
Akiwa katika banda hilo, Prof. Kabudi amesema,ushiriki wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni hatua muhimu inayowapa wananchi fursa ya kupata elimu ya sheria pamoja na huduma za ushauri wa kisheria moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa Serikali.
Ameeleza kuwa,huduma hizo zinachangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya kisheria, haki zao na namna ya kupata msaada wa kisheria kwa wakati, jambo linaloimarisha utawala wa sheria nchini.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James naye alitembelea banda hilo na kupongeza juhudi za Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali za kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi.
Mhe. James amesema,utoaji wa elimu na ushauri wa kisheria katika maonesho hayo unatoa fursa kwa wananchi kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya sheria bila vikwazo, hatua inayochochea uelewa wa sheria na kukuza haki katika jamii.
Kwa upande wake, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba kutoa elimu ya sheria, msaada wa kisheria na ushauri kwa wananchi pamoja na wadau mbalimbali wanaotembelea banda lake.
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yalianza Juni 28,2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13,2026 yakitoa jukwaa kwa taasisi za umma na sekta binafsi kuonesha huduma, bidhaa na ubunifu mbalimbali kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi.
Tags
Habari
Maonesho ya Sabasaba 2026
OAG Tanzania
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Profesa Kabudi
